Mtoto Ramin Ahmed akutwa amefariki dunia

Mtoto Ramin Ahmed mwenye umri wa miaka 3, aliyekuwa anaishi na wazazi wake eneo la Malabi, Kata ya Mpela mkoani Tabora, amepatikana akiwa amefariki dunia katika Kisima kilichopo nyumba waliyokuwa wakiishi.

Awali, familia ya mtoto huyo ilisambaza taarifa kwenye mitandao ya kijamii ikitangaza kumzawadia Sh10 milioni yeyote mwenye taarifa alipo mtoto wao.

Akizungumzia tukio hilo, leo Jumatatu Julai 21, 2025 Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tabora, Richard Abwao amethibitisha kupatikana kwa mtoto Ramin akiwa tayari amefariki ndani ya kisima.

Amesema Julai 18, 2025 saa mbili usiku Ramin alikuwa akicheza na wenzake kwenye kokoto nje ya nyumba yao wakati mama yake akiendelea kupanga vitu walivyokuwa wanahamisha kwenda nyumba nyingine ambapo baada ya muda hakumuona mtoto wake.

"Hii familia ilikuwa kwenye harakati za kuhamisha vitu kwani walikuwa wanahama nyumba hiyo kwenda sehemu nyingine na huyu mtoto pamoja na watoto wengine walikuwa wakicheza mbele ya nyumba yao kwenye kokoto lakini baada ya muda mama alipotoka tena hakumuona mwanaye, ndio akaanza kumtafuta na kuamua pia kutoa taarifa polisi," amesema Kamanda Abwao.

Kamanda huyo amewahimiza wazazi, walezi na jamii kwa ujumla kuweka visima mifuniko pia kuvijengea ili kuepusha majanga kama hayo ambayo yanagharimu uhai wa watoto na haipaswi watoto kucheza karibu na visima vya maji.


Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii