Watu 568 wameokolewa baada ya meli ya abiria ya KM Barcelona 5 kuungua kwa moto baharini nchini Indonesia, ambapo watu watatu wamethibitishwa kufariki dunia, kwa mujibu wa taarifa zilizotolewa na mamlaka za uokoaji leo Jumatatu.
Ajali hiyo ilitokea majira ya mchana jana Jumapili, wakati meli hiyo ikiwa safarini kutoka bandari ya Melonguane katika Wilaya ya Visiwa vya Talaud, kuelekea Manado, mji mkuu wa Mkoa wa Kaskazini mwa Sulawesi.
Kwa mujibu wa Mkuu wa Kituo cha Jeshi la Wanamaji Manado, Kamanda Franky Pasuna Sihombing, moto ulianza ghafla ndani ya meli hiyo na kusababisha hofu kubwa kwa abiria waliolazimika kuruka baharini wakijinusuru.
Katika jitihada za uokoaji, meli ya walinzi wa pwani, boti sita za uokoaji pamoja na boti kadhaa za mpira zilitumika kuwaokoa manusura, Timu za uokoaji ziliweza kuwaokoa watu wengi kutoka baharini, huku wavuvi wa maeneo ya karibu pia wakihusika kuwaokoa baadhi ya abiria waliokuwa wakielea na maboya katika maji ya bahari yaliyokuwa na mawimbi makubwa.
Picha na video zilizosambaa mitandaoni zilionyesha abiria wakiwa na hofu, wengi wao wakiwa wamevaa maboya ya kujiokoa, wakiruka kutoka kwenye meli iliyokuwa ikiwaka moto huku moshi mweusi na moto mkubwa ukionekana.
Taarifa za awali zilieleza kuwa watu watano walifariki, lakini Shirika la Taifa la Utafutaji na Uokoaji limesahihisha idadi hiyo mapema leo Jumatatu na kusema waliothibitishwa kufariki ni watatu tu, baada ya watu wawili waliodhaniwa kuwa wamefariki akiwemo mtoto mchanga wa miezi miwili kuokolewa na kupelekwa hospitalini ambapo walinusurika licha ya mapafu yao kujaa maji ya bahari.