Rais Samia ametangaza kulivunja rasmi Bunge Agosti 3

Rais Samia Suluhu Hassan ametangaza kulivunja rasmi Bunge Agosti 3, mwaka huu, kutoa nafasi ya uteuzi wa wagombea wa nafasi hiyo.

Taarifa ya kuvunjwa kwa Bunge inatolewa katika kipindi ambacho, vyama mbalimbali vya siasa nchini, vipo kwenye hatua za michakato ya ndani ya kuwapata wagombea wa ubunge, urais na udiwani.

Hata hivyo, hati hiyo ya kulivunja bunge imetolewa wakati ambao, zaidi ya wabunge 30 wameenguliwa katika mchakato wa ndani wa Chama cha Mapinduzi (CCM), huku wengine wakisubiri kura za maoni kujua hatima yao.

Hati ya kuvunjwa kwa Bunge hilo imetolewa leo, Jumatano Julai 30, 2025, ikiwa ni utekelezaji wa Ibara ya 92(2)a ya Katiba ya Tanzania inayompa Rais mamlaka ya kulivunja.

Katika hati hiyo, Rais Samia ameandika: "Kwa mujibu wa kifungu cha 49 cha Sheria ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani, Sheria Na. 1 ya Mwaka 2024, uteuzi wa wagombea kwa ajili ya Uchaguzi Mkuu hauwezi kufanyika isipokuwa kama Bunge limekwishavunjwa," imeandikwa hati hiyo.


Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii