Kiongozi mkuu wa upinzani nchini Uganda, Robert Kyagulanyi Ssentamu maarufu kama Bobi Wine, amesema kuwa hali ya kisiasa nchini humo imezidi kuwa mbaya na hatarishi kuelekea Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2026.
Bobi Wine amesema kumekuwa na ongezeko la vitisho dhidi ya maisha yake na wanaharakati wengine wanaoendeleza uhamasishaji wa mabadiliko ya uongozi, hasa kumpinga Rais wa muda mrefu wa taifa hilo, Yoweri Museveni.
"Vitisho dhidi ya maisha yangu vimeongezeka, pamoja na utekaji nyara, kukamatwa kwa watu, na hata mauaji" Alisema.
Aidha, ameitaka jamii ya kimataifa kufuatilia kwa karibu hali ya kisiasa nchini humo, huku akihimiza vijana na wananchi kwa ujumla kujiandaa kushiriki uchaguzi ujao kwa amani lakini kwa uthabiti wa kudai haki zao za kidemokrasia.
Mashirika ya haki za binadamu yameelezea wasiwasi wao kuhusu mazingira ya kisiasa nchini Uganda, wakitaka uchaguzi wa 2026 ufanyike kwa uhuru, haki na usawa kwa vyama vyote.