Ndoto za waliokuwa wabunge wa Viti Maalum Mkoa wa Arusha, Catherine Magige na Zaytun Swai, kurejea bungeni zimetumbukia nyongo, baada ya kushindwa kuwashawishi wajumbe wa Umoja wa Wanawake wa Chama Cha Mapinduzi (UWT) Mkoa wa Arusha katika mchujo wa kura za maoni uliofanyika mjini Arusha.
Katika uchaguzi huo uliomalizika usiku wa kuamkia Julai 31 mwaka huu Martha Gido aliibuka kidedea kwa kupata kura 1,004, akifuatiwa na Chiku Athman aliyepata kura 775 kati ya kura halali 1,245 zilizopigwa.
Waliokuwa wabunge wa viti maalum, Magige na Swai, walipata kura 213 na 141 mtawalia, matokeo yanayowaweka njia panda katika safari yao ya kisiasa kuelekea Bunge. Wagombea wengine waliojibwaga uwanjani ni Asanterabi Lowassa (kura 196), Navoi Mollel (95), Martha Amo (50), na Lilian Badi (9).
Akizungumza wakati wa kutangaza matokeo, Mkuu wa Mkoa wa Arusha Kenani Kihongosi, ambaye pia alikuwa msimamizi wa uchaguzi huo, amebainisha kuwa jumla ya wapiga kura walikuwa 1,261, na kura halali 1,245 huku kura saba zikiharibika. Ikumbukwe kuwa wajumbe wanaopiga kura wanatakiwa kupiga kura zaidi ya moja kwa maana ya kuwapigia wagombea wawili ambao ndio huibuka kidedea katika nafasi hizo za viti maalumu kwa mkoa.
Aidha amebainisha kuwa uchaguzi umefanyika kwa utulivu na demokrasia huku akisisitiza mshikamano na umoja baada ya matokeo hayo.
Katika hotuba yake baada ya kutangazwa mshindi, Martha Gido, amewashukuru wajumbe kwa kuonesha imani kwake, na kuahidi kuwa mtetezi wa wanawake, vijana na jamii kwa ujumla.