Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imetoa msamaha wa kodi kwa wamiliki wa magari yasiyokidhi matakwa ya forodha kwa kipindi cha kuanzia Agosti mosi hadi Disemba 31 mwaka huu.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na TRA leo Agosti Mosi Jijini Dar es Salaam na kusainiwa na Kamishna Mkuu Bw. Yusuph Juma Mwenda imeeleza kuwa katika kipindi cha msamaha, wamiliki wa magari husika watawajibika kulipa kiasi cha ushuru na kodi husika, bali kiasi cha riba na adhabu vyote vitasamehewa.
Taarifa hiyo imesema TRA katika kutekeleza majukumu yake yaliyokasimiwa kwa mujibu wa Sheria ya Mamlaka ya Mapato Tanzania, Sura 399 (kama ilivyofanyiwa marejeo), imekuwa ikikabiliana na changamoto za usimamizi wa magari yasiyokidhi matakwa ya Sheria ya Forodha (uncustomed vehicles), ambayo hayakulipiwa ushuru na kodi husika wakati wa kuingizwa nchini.
Pia, Magari yaliyoingizwa nchini kwa muda (temporary importation) na hayakuweza kurudishwa yalikotoka.
Vilevile,Magari yaliyoingia Tanzania Bara kutokea Zanzibar bila kufuata taratibu za kiforodha, magari yaliyoingizwa nchini kwenda nchi nyingine (transit) na yakabakizwa au kutelekezwa nchini.