Mnamo Agosti 2 mwaka huu watia nia wa nafasi za udiwani katika Wilaya ya Rufiji, mkoani Pwani, wameandamana hadi katika ofisi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Kata ya Umwe, wakilalamikia kukiukwa kwa maelekezo ya Sekretarieti ya Halmashauri Kuu ya CCM Taifa kuhusu mchakato wa uteuzi wa wagombea wa nafasi hizo.
Licha ya agizo rasmi lililotolewa na CCM Taifa mnamo Julai 31 mwaka huu likielekeza kuwa wagombea wote wa udiwani waliokuwemo kwenye orodha ya awali warejeshwe kwa ajili ya kupigiwa kura za maoni, majina hayo yameelezwa kutorudishwa kwa utekelezaji katika baadhi ya kata wilayani Rufiji- jambo ambalo limezua sintofahamu na taharuki kwa baadhi ya wagombea na wanachama wa chama hicho.
Katika hali isiyo ya kawaida, baadhi ya watia nia wamesema wamebaki na maswali yasiyo na majibu juu ya kwanini maelekezo ya chama kwa ngazi ya juu yamepuuzwa ngazi ya wilaya, hali inayozua hisia za upendeleo na kuhujumu mchakato wa kidemokrasia ndani ya chama.
Agizo la CCM Taifa lilitolewa na CPA Amos Gabriel Makalla, Katibu wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa anayeshughulikia Itikadi, Uenezi na Mafunzo, kufuatia kikao cha sekretarieti kilichofanyika Julai 31, 2025. Katika taarifa hiyo, CCM ilibatilisha maamuzi yote ya awali kuhusu uteuzi wa wagombea wa udiwani na kuamuru mchakato wa kura za maoni urejeshwe kwa haki na uwazi.
“Wagombea wote wa udiwani wa kata, waliopitishwa na Kamati za Siasa za Mikoa warejeshwe ili wakapigiwe kura za maoni…wagombea wote waliopo kwenye orodha ya awali waliyotumiwa Makatibu wa Mikoa wa CCM, warejeshwe ili wakapigiwe kura za maoni”, ilisema taarifa hiyo.