Wakati hali ya uchumi ikiendelea kuzorota na mfumuko wa bei ukielekea asilimia 30, vigogo wawili wa siasa nchini Malaw- marais wa zamani Peter Mutharika na Joyce Banda wamezindua kampeni zao Jumapili kwa ajili ya uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Septemba 16 mwaka huu.
Katika taifa hilo dogo la kusini mwa Afrika lenye watu milioni 21, kinyang'anyiro cha urais kinatarajiwa kuamuliwa na masuala ya njaa, ukosefu wa ajira, na kupanda kwa gharama za maisha.
Akiwahutubia maelfu ya wafuasi wake katika jiji la pili kwa ukubwa nchini humo, Blantyre, Mutharika (85), ambaye anaongoza chama kikuu cha upinzani cha Democratic Progressive Party (DPP), aliahidi kuikomboa Malawi kutoka kwenye kile alichokitaja kama “mateso ya kisiasa na kiuchumi”.
“Leo hii, Malawi iko katika mateso – njaa, umasikini, na hofu dhidi ya serikali ambayo ilipaswa kutulinda. Tunapaswa kuiheshimu serikali, si kuogopa,” amesema Mutharika.
Mutharika aliongoza Malawi kuanzia mwaka 2014 hadi 2020, lakini ushindi wake katika uchaguzi wa 2019 ulifutwa na mahakama kutokana na kasoro katika mchakato wa kura. Tangu hapo, amekuwa mshindani mkuu wa Rais Lazarus Chakwera wa Malawi Congress Party (MCP).
Viongozi wa upinzani wameendelea kuilaumu serikali ya Chakwera kwa “kukandamiza sauti za upinzani” na kushindwa kurekebisha hali ya maisha ya wananchi.
Katika mwezi wa Juni maandamano madogo yaliyokuwa yakishinikiza ukaguzi huru wa daftari la wapiga kura yalivamiwa na watu wasiojulikana. Wapinzani walituhumu wafuasi wa chama tawala kuhusika, tuhuma ambazo serikali imezipinga.
Wakati huo huo, aliyekuwa rais mwanamke wa kwanza nchini humo, Joyce Banda (74), alizindua rasmi kampeni yake katika mji wa Ntcheu, katikati mwa Malawi. Banda ni mwalimu na mwanaharakati wa haki za wanawake, na sasa anaongoza chama cha People’s Party.
Katika hotuba yake, amesisitiza kuwa ajenda yake kuu ni “uwezeshaji wa vijana na uundaji wa ajira.”
“Malawi haiwezi kuendelea kuwa nchi ya watu wanaota bila matumaini. Vijana wetu wanahitaji ajira na fursa halisi za maisha,” amesema Banda.
Banda alichukua uongozi mwaka 2012 baada ya kifo cha aliyekuwa rais Bingu wa Mutharika, lakini alishindwa katika uchaguzi wa mwaka 2014.