Wadau wa Afya watakiwa kushirikiana na Serikali kuboresha huduma za lishe

Wadau wa Sekta ya Afya wametakiwa kushirikiana na Serikali ili kuboresha huduma za lishe kwa kuwekeza kwenye upatikanaji wa mashine za urutubishaji wa vyakula hapa nchini.

Wito huo umetolewa  Agosti 14 mwaka huu na Waziri wa Afya Mhe. Jenista Mhagama wakati wa hafla fupi ya makabidhiano ya gari iliyotolewa na Taasisi isiyo ya Serikali ya SANKU kwa ajili ya utekelezaji wa usimamizi na ufuatiliaji wa program ya urutubishaji wa vyakula nchini.

“Tunahitaji kuendelea kushirikiana katika kuboresha huduma za lishe bora, tunahitaji sana mashine zinazotumika kuchanganyia virutubishi kwenye vyakula, pamoja na ushirikiano wa kupata vifaa vitakavyotusaidia kufikia malengo ya kitaifa ikiwemo huduma ya usafiri,” amesema Waziri Mhagama.

Waziri Mhagama amesema ili kuwa na Taifa lenye ukomavu na mwendelezo wa akili na ubora wa watoto tulionao ni lazima watoto wale chakula chenye ubora, wajawazito pia watumie lishe bora ili kupunguza vifo vitokanavyo na uzazi.

Waziri Mhagama amesema Serikali imeendelea kuboresha huduma za lishe nchini na sasa Tanzania ina kiwanda cha kwanza cha uzalishaji wa virutubishi hapa nchini

“Tumeweka historia ndani ya nchi, Tanzania ina kiwanda cha kwanza cha uzalishaji wa virutubishi na sasa tumeanza uzalishaji hapa nchini, tukiwezesha watoto wetu kupata chakula chenye lishe bora tutatuwa tumewekeza kwenye maendeleo ya taifa kwa ujumla,” amefafanua.

Kwa upande wake Mkurugenzi Msaidizi Huduma za Lishe Bi. Neema Joshua amesema Serikali imetoa mwongozo wa kusimamia programu hiyo ya kuongeza virutubishi katika unga, mafuta na chumvi.

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii