Vijana wa Chama cha Ukombozi wa Umma (CHAUMMA) Wilaya ya Same Mkoani Kilimanjaro wameeleza kuwa wapo radhi kutoa kadi zao za kupiga kura kwa mgombea wao ili wawe na uhalali wa kujipigia kura wenyewe kutokana na kuridhishwa na sera yao ya utoaji wa ubwabwa.
Wakizungumza hivi karibuni mara baada ya mtiania wa Ubunge kupitia CHAUMMA Gervas Mgonja kurejesha fomu zoezi lililoambatana na ufunguzi wa ofisi za chama hicho Same Mjini, baadhi ya vijana wameeleza kuwa sera ya chama hicho ya kutoa chakula ni ishara tosha ya uzalendo na kujali wananchi wake.
"Nampa kadi yangu akajipigie kura kuanzia Diwani, kama wanajali afya ya mtanzania kwa kula wewe ni Mtanzania mzalendo, uzalendo unaanzia pale unapojali afya ya mtu, kama utanipa hela na mimi sijala nina njaa, nitaenda kunywa pombe kama umenipa chakula inamaana umejali afya yangu na mimi nitakubali" walieleza vijana hao.
Itakumbukwa kuwa kifungu cha 88 cha Sheria ya Taifa ya Uchaguzi kinasema kuwa ni kosa la jinai kwa mtu kuchukua kadi ya mpiga kura mwingine na kuizuilia, kukataa kuirudisha au kubaki nayo kwa uzembe.Vilevile Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) imekuwa ikiwatahadharisha watu wanaochukua kadi za kupigia kura za wenzao na kuzizuilia au kubaki nazo kuwa ni kinyume cha Sheria.