Bodi ya Utalii Tanzania Bara (TTB) na
Kamisheni ya Utalii Zanzibar (ZCT) zimeendelea kufanyakazi kwa pamoja
katika eneo la Utangazaji wa utalii nchini.
Ambapo imeelezwa
kuwa, utalii una mchango mkubwa katika uchumi wetu. Takwimu zinaonyesha
kuwa kwa mwaka 2019/2020 utalii ulichangia asilimia 17.2 katika pato la
Taifa la Tanzania Bara na asilimia 27 upande wa Zanzibar.
Akizungumza
jana akiwa Visiwani Zanzibar, Msemaji Mkuu wa Serikali na Mkurugenzi wa
Idara ya Habari – MAELEZO, Gerson Msigwa wakati akitoa taarifa ya wiki
kuhusu utekelezaji wa miradi ya Serikali katika maeneo mbalimbali
nchini, alisema kuwa sekta hii imekumbwa na changamoto kubwa ya Janga la
Uviko-19 lakini juhudi za kukabiliana na changamoto hizo zimeendelea
kuzaa matunda ambapo mwaka 2020 watalii walikuwa 620,867 na sasa
wameongezeka hadi kufikia watalii 922,692 Bara na Visiwani.
“Tumepata
changamoto ya janga la ugonjwa wa Korona (Uviko-19) ambapo sekta hii
imeathirika na kusababisha idadi ya Watalii kushuka kutoka 1,527,230
waliotembelea Tanzania mwaka 2019 hadi 620,867 mwaka 2020. Hata hivyo
juhudi tulizozifanya za kuchukua tahadhari dhidi ya ugonjwa huo na
kuwavutia zaidi watalii tumefanikiwa kuanza kuongeza idadi ya watalii
ambapo katika mwaka 2021 idadi imeongezeka hadi kufikia 922,692,”
alisisitiza Msigwa.
Aidha amesema kuwa, TTB na ZCT zimeendelea
kufanya jitihada mbalimbali katika kuratibu na kushiriki kuandaa
maonesho ya Kimataifa ya Utalii, mfano ni Onesho la Utalii la Jumuiya ya
Afrika Mashariki (EAC Tourism Expo) lililofanyika Arusha kwa mafanikio
makubwa na Dubai Expo 2020 ambayo inaendelea huko Dubai.
Vilevile,
kumekuwepo na ushirikiano wa Sekta Binafsi, Wafanyabiashara wa Sekta ya
Utalii wa Bara na Zanzibar (Tour Operators) ambao wanafanya kazi pamoja
hasa katika kupokea wageni na kuuza safari kwa wageni wanaokuja
kutembelea vivutio vya utalii nchini.