Ikiwa leo Septemba 22 ni siku ya kumbukizi juu ya uhifadhi wa faru duniani Serikali kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii imeendelea na jitihada mbalimbali za kuendeleza miradi mbalimbali ya uhifadhi wa wanyama aina ya Faru katika hifadhi ya Taifa ya Mkomazi kitu ambacho kimevutia watalii wengi kutembelea Hofadhi hiyo maarufu kwa Faru weusi.
Hayo yamebainishwa Septemba 22 mwaka huu na Mhifadhi Daraja la kwanza na Msimamizi wa Faru weusi Jackson Limo ikiwa ni siku moja kuelekea siku ya Faru Duniani ambapo amebainisha miradi hiyo ikiwa ni pamoja na mradi wa Sima na Mradi wa Mbura Rhino Chenchure
“Serikali kwa kushirikiana na wadau ilianza kurejesha Faru weusi na Mbwa Mwitu katika hifadhi ya Taifa ya Mkomazi kuanzia mwaka 1997 kutoka Afrika ya Kusini, Bara la Ulaya na kwenye mashamba mengine ya wanyama ili kutimiza shauku ya watalii wanaokuja kutembelea hifadhi hii” alisema Limo
Amesema mpaka sasa kuna miradi miwili mradi wa Kisima ambao ni wa uzalishaji na mradi wa Mbura kwa ajili ya utalii.
Tulianza na mradi wa Kisima ambao ni wa uzalishaji lakini tuliona ipo haja kuongeza mradi mdogo kwa ajili ya Utalii ili kutimiza lengo la wageni wanaotaka kuona Faru kwa karibu zaidi’ alisema.
Aidha Serikali kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii inaendelea na mikakati ya makusudi ya kiulinzi na usalama wa ikolojia ya wanyama hao ili kuweza kuzaliana zaidi na kupelekwa kwenye hifadhi nyingine kuongeza msukumo wa utalii wa Faru kwenye hifadhi zote zilizopo hapa nchini
Itakumbukwa Septemba, 22 kila mwaka Tanzania huungana na Mataifa mengine Ulimwenguni kuadhimisha Siku ya Faru duniani kwa lengo la kutambua, kuthamini na kuongeza uelewa kwa jamii ya juu ya umuhimu na thamani ya uhifadhi wa Faru kwa pato la taifa kupitia shughuli za utalii.