Mgombea ubunge kupitia Chama cha ACT Wazalendo, Jimbo la Nanyumbu, Hamad Hasheem ametangaza kuhamia Chama cha Mapinduzi (CCM), huku akisema amevutiwa na mienendo na mwonekano wa chama hicho baada ya kuangalia mikutano ya mgombea urais wa chama hicho, Samia Suluhu Hassan na kugundua kuwa anaweza.
Amesema hayo leo Septemba 23 mwaka huu kwenye kampeni za mgombea urais wa CCM, Samia akiwa Mangaka, Wilaya ya Nanyumbu mkoani Mtwara.
"Ndugu zangu ninasema Samia anaweza, nimepata majibu leo, nimepata majibu Kigoma nilikuwa nafuatilia kampeni za mama Samia, Nimeridhika kwa moyo wa dhati," amesema.
"Nilifikiri miradi mikubwa aliyoacha Hayati John Magufuli, mradi wa Busisi mama kapita nalo, ameleta vichwa vya treni vya kisasa. Daraja la Busisi limenifanya niamini kuwa katika ukanda wa Afrika Mashariki sidhani kama ana mwenzake," amesema Hasheem.
"Leo ninatangaza nakihama Chama cha ACT Wazalendo, navaa jezi ya kijani na njano naombeni mnikaribishe," amesema.