Kaimu RC Kazungu: Tanzania imepiga hatua kubwa usimamizi wa rasilimali madini*
Wizara, Tume ya Madini zatoa elimu ya madini kwa ujumbe kutoka Malawi
Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Dodoma ambaye pia ni Katibu Tawala wa Mkoa huo Dkt. Khatibu Kazungu amepokea ujumbe maalum kutoka nchini Malawi uliowasili nchini Tanzania kwa lengo la kujifunza na kubadilishana uzoefu katika masuala mbalimbali ya usimamizi wa rasilimali madini.
Ujumbe huo, umeongozwa na Mtendaji Mkuu wa Maendeleo ya Biashara ya Vikundi Zizwan Khonje akiwa ameongozana na wadau wa Sekta ya Madini akiwemo Rais wa Shirikisho la Vyama vya Wachimbaji Wadogo wa Malawi na maafisa mbalimbali wa mabenki wa nchini humo na kupokelewa rasmi katika Ofisi za Mkuu wa Mkoa jijini Dodoma, ambapo umeeleza dhamira yake ya kujifunza kutoka Tanzania kutokana na mafanikio makubwa iliyoyapata katika kusimamia sekta ya madini kwa uwazi, tija na mchango wake katika uchumi wa Taifa.
Akizungumza wakati wa kuupokea ujumbe huo, Dkt. Kazungu amewapongeza wageni hao kwa kuichagua Tanzania kama kituo cha maarifa na uzoefu katika sekta ya madini huku akisisitiza kuwa hatua hiyo ni ishara ya kutambua jitihada kubwa zinazofanywa na Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, katika kuboresha mazingira ya uwekezaji na kuleta mageuzi katika sekta hiyo muhimu.
“Kwa niaba ya wananchi wa Mkoa wa Dodoma na Serikali ya Tanzania, nawakaribisha kwa moyo mkunjufu. Uamuzi wenu wa kuja kujifunza kwetu ni ushahidi wa wazi kuwa tunapiga hatua kubwa katika usimamizi bora wa rasilimali zetu, hasa madini. Hili ni jambo la kujivunia kama taifa,” amesema Dkt. Kazungu.
Dkt. Kazungu ameeleza kuwa Tanzania, kupitia Wizara ya Madini na taasisi zake imefanikiwa kujenga mifumo imara ya usimamizi wa shughuli za utafutaji, uchimbaji, biashara, na usafirishaji wa madini, huku ikizingatia kanuni za uwazi, uwajibikaji na ushirikishwaji wa wananchi katika maeneo yanayozungukwa na shughuli za madini.