Mkuu wa Chuo cha Taaluma ya Polisi Dar es Salaam Naibu Kamishna wa Polisi (DCP) Dkt. Lazoro B. Mambosasa, amewataka maafisaĜwakaguzi na askari kuendelea kuwa wazalendo katika kutunza mali za Jeshi la Polisi zinazotolewa na serikali kwa gharama kubwa ili ziendelee kutoa huduma bora kwa jamii.
DCP. Dkt. MAMBOSASA amesema hayo katika mapokezi ya gari mpya ya kisasa aina ya TATA (Macopollo) Septemba 24 mwaka huu lililonunuliwa na Chuo hicho kwa ajili shule ya udereva Kilwa Road (VTC) Academy Driving School ambapo kitatoa mafunzo ya udereva wa abiria (PSV).
Dkt. Mambosasa amesema basi hilo litasaidia kuwanoa na kuwajengea uwezo madereva kuwa mahiri wenye ujuzi na weledi wanaokwenda kuhudumia wasafiri wakiwa wanajiamini na kutoa huduma bora.
Dkt. Mambosasa amewakumbusha kusimamia mafunzo kwa weledi na kutoa madereva mahiri ili kuzuia na kudhibiti ajali za barabarani zinazotokea kwa uzembe na kuleta madhara kwa watu na miundombinu mingine.
Kwa upande wake Mkuu wa Mafunzo chuo cha Taaluma ya Polisi Dar es Salaam ACP Andrea G. Legembo amesema yeye na wakufunzi anaowasimamia watahakikisha wanatunza gari hilo na kufundisha kwa mujibu wa Sheria,taratibu,kanuni na miongozo inayohusu madereva wa abiria ili kutoa madereva wanaozingatia Sheria za barabarani na kuhakikishia watumiaji wengine wa barabara kuwa salama.
Mkuu wa kitengo cha udereva Mrakibu Mwandamizi wa Polisi (SSP) Deus Sokoni, ameahidi kuendelea kutoa elimu ya usalama barabarani kwa madereva na kuwajengea uelewa wa masuala ya sheria na umuhimu wa utoaji huduma bora kwa mteja na hivyo kupunguza malalamiko.