Loveness atiwa hatiani kwa kosa la kujiteka mwenyewe

Jeshi la Polisi Mkoa wa Mwanza linamshikilia Loveness Daniel Kisile (30), mkazi wa mtaa wa Temeke kata ya Mhandu wilayani Nyamagana kwa kosa la kutoa taarifa za uongo kwa mume wake na ndugu zake akidai ametekwa na watu watatu wa kiume waliotaka kumdhuru na kutoa ujauzito wake endapo wasingepewa shilingi milioni kumi.

 Akizungumzia tukio hilo Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza DCP Wilbroad Mutafungwa amesema tukio hilo lilitokea usiku wa Septemba 24 mwaka huu ambapo inadaiwa mtuhumiwa alimwapigia simu mume wake Hosea Joel Lusigwa akidai ametekwa na baadaye akadai mimba yake ya mapacha watatu imetolewa kisha kuendelea kusisitiza fedha zitumwe ili aachiliwe huru hali iliyosababisha taharuki kubwa kwa familia na jamii.

 Mara baada ya Upelelezi kufanyika na jeshi la polisi walifanikiwa kumkamata mtuhumiwa Septemba 25 mwaka huu alfajiri katika mtaa wa Mecco kata ya Buzuruga akiwa salama huku uchunguzi wa kitabibu ukibaini hakuwa na ujauzito na baada ya kukiri kosa alikiri kutoa taarifa hizo za uongo kwa lengo la kumdanganya mume wake na wakwe zake ili kupata fedha kwa manufaa yake binafsi ambapo Jeshi la Polisi limeonya wananchi kuacha vitendo hivyo na kuwataka kuzingatia ukweli kwani yeyote atakayebainika atachukuliwa hatua kali za kisheria. 

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii