Madaktari bingwa na wataalamu wa afya kutoka Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Ziwa-Bugando kwa kushirikiana na Zahanati ya Polisi Mabatini, wameendesha kliniki maalum ya uchunguzi wa magonjwa ya saratani kwa askari wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Mwanza na familia zao.
Uchunguzi huo umefanyika Septemba 24 mwaka huu katika Zahanati ya Polisi Mabatini, jijini Mwanza, ambapo huduma mbalimbali za kiafya zilitolewa, ikiwemo upimaji wa saratani ya ini, matiti, shingo ya kizazi kwa wanawake, pamoja na tezi dume kwa wanaume.
Akizungumza wakati wa utoaji wa huduma hizo, Dkt. Erica Mgonja kutoka Hospitali ya Bugando alisema lengo kuu la kampeni hiyo ni kutoa huduma za kinga kabla ya tiba kwa askari na familia zao, huku akisisitiza umuhimu wa upimaji wa afya mara kwa mara hata kama hakuna dalili za ugonjwa.
“Saratani nyingi hazionyeshi dalili mapema. Askari wetu wanakumbana na mazingira yenye msongo wa kazi, hivyo ni muhimu afya yao kufuatiliwa kwa ukaribu kwa ustawi wao na wa familia,” alieleza Dkt. Mgonja.
Kwa upande wake, Mkuu wa Polisi Kikosi cha Afya Mkoa wa Mwanza, Mrakibu wa Polisi (SP) Dkt. Stephen Kisaka, aliipongeza Hospitali ya Bugando kwa ushirikiano na kujali ustawi wa afya za askari na familia zao.
“Tumejipanga kuendeleza huduma hizi kwa kushirikiana na wadau mbalimbali. Afya bora kwa askari ni msingi wa ufanisi katika utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku,” alisema SP Kisaka.
Askari waliopatiwa huduma hizo waliwashukuru madaktari na wahudumu wa afya kwa kutambua umuhimu wa kinga, wakisema hatua hiyo imewajengea mwamko wa kujitunza kiafya kwa wakati.
Jeshi la Polisi Mkoa wa Mwanza linaendelea kushirikiana na sekta ya afya kuhakikisha ustawi wa askari na familia unalindwa, sambamba na kuhamasisha jamii kuhusu umuhimu wa huduma za uchunguzi wa afya kwa wakati.