Mpina apewa siku 14 kupinga maamuzi ya Msajili

Mahakama Kuu ya Tanzania (Masjala Kuu Dodoma) imetoa kibali kwa Chama cha ACT Wazalendo na Ndugu Luhaga Joelson Mpina kufungua shauri la kupinga maamuzi ya Msajili wa Vyama vya Siasa na Mwanasheria Mkuu wa Serikali kuondoa jina la Mpina.

Kwa mujibu wa taarifa rasmi iliyotolewa na kusainiwa leo Septemba 26 mwaka huu na Mwanasheria Mkuu wa Chama cha ACT Wazalendo, Mahakama hiyo chini ya Jaji Wilbert Chuma imeridhia maombi hayo baada ya kutimiza vigezo vyote vinavyohitajika kisheria pamoja na misingi iliyowekwa na maamuzi ya awali ya Mahakama ya Rufaa ya Tanzania.

ACT Wazalendo na Luhaga Mpina wana siku 14 kuanzia leo za kuwasilisha rasmi maombi ya kufutwa kwa maamuzi hayo ya Msajili wa Vyama vya Siasa na Mwanasheria Mkuu wa Serikali.

Aidha, chama cha ACT Wazalendo kimeendelea na shauri la Kikatiba nambari 24027 dhidi ya Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) na Mwanasheria Mkuu wa Serikali. Shauri hilo litasikilizwa Septemba 29 mwaka huu mbele ya majaji watatu ambao ni Jaji Frederick Manyanda, Jaji Sylvester Kainda na Jaji Abdallah Gonzi.

Itakumbukwa kuwa Msajili wa Vyama vya Siasa na Mwanasheria Mkuu wa Serikali waliwasilisha mapingamizi wakitaka maombi hayo yatupiliwe mbali kwa hoja kwamba yanapingana na misingi ya kisheria. Hata hivyo, Mahakama iliona mapingamizi hayo hayana msingi na kuyatupilia mbali.

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii