Balozi wa China nchini Chen Mingjian amesema nchi zinazoendelea ikiwemo Tanzania zinaweza kuondokana na umaskini iwapo watu wake watakuwa na uvumilivu,ustahimilivu na kufanya kazi kwa bidii bila kuchoka.
Balozi huyo aliyasema hayo wakati wa uzinduzi wa toleo la Kiswahili la kitabu cha Rais Xi Jinping, Kupanda na Kutoka Kwenye Umaskini,lililofanyika jijini Dar es Salaam mwishoni mwa wiki.
Alisema kuwa toleo hili la Kiswahili limeandaliwa kwa ushirikiano kati ya Serikali ya China na Mkuki na Nyota Publishers, kwa lengo la kuwasaidia Watanzania na nchi nyingine za Afrika kupata uzoefu na mbinu za vitendo kutoka katika historia ya China ya kupambana na umaskini.
Alisema kitabu kimekusanya hotuba 29 na ripoti za utafiti zilizotolewa na Xi Jinping alipokuwa Katibu wa Chama cha Kikomunisti katika Wilaya ya Ningde, Mkoa wa Fujian, kati ya mwaka 1988 na 1990.
Wakati huo, eneo hilo lilikuwa miongoni mwa maskini zaidi nchini China, na uongozi wa Xi ulilenga kuhamasisha jamii, kufanya mageuzi ya vijijini, na kuanzisha sera zilizoboreshwa moja kwa moja maisha ya wananchi.
Balozi Mingjian alisema kitabu kinaakisi falsafa ya maendeleo yenye kumlenga mwananchi ya Chama cha Kikomunisti cha China na kuonyesha imani ya Xi katika kusaidia maeneo yaliyoathiriwa na umaskini.
“Ufanisi wa China unatokana na kuelewa mazingira yake ya kitaifa na mantiki ya utawala wa kupambana na umaskini,” alisema
Alibainisha kuwa China ilitimiza malengo ya Umoja wa Mataifa ya kupunguza umaskini ya mwaka 2030 miaka kumi kabla ya muda uliopangwa, hatua iliyozipa moyo mataifa mengi yanayoendelea.
Balozi Mingjian aliongeza kuwa toleo la Kiswahili litakuwa daraja la mawazo, likishirikisha uzoefu wa China na Tanzania pamoja na Afrika, huku kila nchi ikihimizwa kutumia mafunzo hayo kulingana na hali yake.
Aliyekuwa Katibu Mkuu wa CCM, Wilson Mukama, alisema mapambano dhidi ya umaskini Afrika lazima yaanze kwenye fikra.
“Ni lazima kwanza tuondoe umaskini wa mawazo. Kila eneo lina changamoto zake, na suluhisho lazima zibuniwe mahsusi kwa ajili yake,”
Aliyekuwa Mkurugenzi wa Mkuki na Nyota Publishers, Walter Bgoya, alisisitiza umuhimu wa uongozi wenye dira.
“Miujiza haitoki tu angani. Huanzia kwa kiongozi mwenye uwajibikaji anayeweza kuhamasisha wananchi wake kufanya kazi kwa bidii,” alisema Bgoya
Bgoya aliongeza kuwa uthabiti wa Tanzania, sambamba na msaada wa China katika sekta za kilimo, elimu na miundombinu, unatoa mazingira wezeshi kwa juhudi za kupunguza umaskini.
Alisisitiza kuwa uvumilivu, ubunifu na ushiriki wa jamii ni muhimu iwapo Afrika inataka kuharakisha maendeleo jumuishi na kufanikisha ustawi endelevu.