Wadau wataja mambo 20 kuimarisha demokrasia nchini Tanzania

WADAU wa demokrasia nchini, wamependekeza zaidi ya mambo 20 wanayoamini yakifanyiwa kazi yanaweza kuimarisha umoja na mshikamano nchini.

Wadau hao walitoa mapendekezo hayo juzi jijini Dar es Salaam katika kilele cha maadhimisho ya siku ya demokrasia duniani.

Miongoni mwa mapendekezo hayo ni kutaka ushiriki wa wanawake uimarishwe katika uongozi na mchakato wa uamuzi katika ngazi zote, kuanza kwa mchakato wa kupatikana Katiba mpya itakayotokana na maoni ya wananchi.

Mengine ni kufanyike kwa maboresho ya kisera na kisheria ili kukuza ushiriki wa wanawake katika masuala ya kisiasa na uongozi, kuondoa vikwazo kwa raia kuzifikia taasisi zinazotoa huduma, kutoa maoni na kupata taarifa.

Kuendelea kukuza ushiriki wa wananchi na kuendelea kutoa maoni yao bila kuogopa, kufanyike maboresho katika Katiba maeneo yanayotishia haki za kidemokrasia na kutoa haki kwa kuangalia upande.

Pia, walipendekeza Katiba ijayo itoe nafasi kwa mgombea binafsi, ushirikishwaji wa wadau katika utungaji sera, wananchi wawe na uwezo wa kuwaondoa viongozi kabla ya uchaguzi mwingine.

Kadhalika, Bunge lirekebishe Sheria za Huduma za Habari iendane na viwango vya mataifa, kuangaliwe sheria za kuminya uhuru wa kujumuika kwa mashirika yasiyo ya kiserikali na kuondoa urasimu kwa mashirika yanayotaka usajili. 

Wadau hao walisema, Tume Huru ya Uchaguzi (INEC) ina nafasi ya kuleta demokrasia na kukuza ushiriki wa wanawake katika siasa, lakini inapaswa kupewa mamlaka ya kusimamia ipasavyo kanuni na sheria zake. 

Katika maadhimisho hayo, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Wakili Fulgence Massawe, alisema demokrasia imara haiwezekani bila sauti za wanawake kusikika, kushiriki na kupewa nafasi sawa.

Alisema demokrasia inakuwa imara zaidi sauti za wanawake zinaposikika na ushiriki wa kila mtu ni msingi wa demokrasia thabiti.

"Tuna mazingira jumuishi ya kidemokrasia na kuimarisha ushiriki wa wanawake katika uongozi na mchakato wa uamuzi katika ngazi zote," alisema Wakili Massawe.

Kaulimbiu ya maadhimisho ya mwaka huu inasema; 'Kukuza sauti za wanawake kwa ustahimilivu wa demokrasia’, amabayo inaonesha jinsi wanawake walivyo na umuhimu kwenye masuala ya uongozi.

Alisema demokrasia ni kielelezo cha ustawi wa haki za binadamu, pia ni ishara ya kuendeleza utamaduni wa ustaarabu na utii wa sheria, na uwapo wa demokrasia ni kiashiria cha utekelezaji wa dhana ya ushiriki na ushirikishwaji wa wananchi katika kufanya maamuzi ya kuchagua viongozi wao.

“Sisi Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), tumeandaa maadhimisho haya na kushirikisha wadau mbalimbali wa haki za binadamu ili kupata mapendekezo ya pamoja tutakayo yafikisha kwa viongozi ili yafanyiwe kazi," alisema Wakili Massawe.

Mchambuzi wa masuala ya siasa, Deus Kibamba alisema Katiba mpya ni hitaji la muda mrefu la Watanzania ambalo likitekelezwa litapunguza vilio vyao.

"Kwa kuwa viongozi wametuahidi kutekeleza hitaji hilo, basi ni vyema lifanyiwe kazi ili Watanzania wapate kile ambacho kimekuwa ni tamanio lao," alisema Kibamba.

Alisema kwa kuwa serikali imeshaahidi kufanya mchakato wa kupatikana Katiba hiyo, anaamini hilo litafanyika ili kuwa na inayokubalika kwa wote.

“Katiba mpya itaongeza ushiriki wa wananchi katika demokrasia kuliko iliyopo sasa ambayo imejaa viraka vingi, hivyo, ni matumaini yangu kuwa viongozi watatimiza ahadi ya kuwapa Watanzania katiba mpya," alisema.

Mwenyekiti wa Jukwaa la Katiba (JUKATA), Dk. Ananilea Nkya. alisisitiza upatikanaji wa Katiba mpya ili isaidie dhidi ya vitendo vya uhalifu na kuimarisha utawala bora.

Alisema ipo haja kwa Watanzania kupewa elimu juu ya athari za kiuchumi zitokanazo na Katiba iliyopo, na kwamba fedha nyingi zinatumika katika kuendesha mambo ambayo kama ingekuwapo yasingefanyika.

"Pamoja na hayo, katiba mpya italeta usawa wa kijinsia katika uongozi, kwani viti maalum ni matumizi mabaya ya fedha za umma," alisema Dk. Ananilea.

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii