KATIKA miji mikuu inayozidi kukua kwa kasi kama Dar es Salaam, ndoto za mafanikio zinaambatana na hali halisi inayoleta madhara kimyakimya kwa afya ya wakazi wake, mojawapo ikiwa ni kukosa usingizi wa kutosha.
Wakazi wengi wa jiji hili linalokadiriwa kuwa na zaidi ya watu milioni 5.383 kwa mujibu wa Sensa ya Watu na Makazi ya Mwaka 2022), wanajikuta wakilala kwa saa chache mno. Waathirika wakuu ni wafanyakazi na wanafunzi.
Kuamka alfajiri na kuchelewa kurudi nyumbani kwa sababu ya foleni, miundombinu ya usafiri isiyotosheleza, na shinikizo la maisha ya kila siku, vimefanya usingizi kuwa kama bidhaa ya kifahari inayopatikana kwa nadra.
Je, athari za ukosefu wa usingizi ni zipi? Na kwa kiasi gani watu wanapuuza hitaji hili la msingi kwa afya ya mwili na akili?
USINGIZI NI CHAKULA
Kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO), mtu mzima anapaswa kulala kati ya saa saba hadi tisa kwa usiku ili kuhakikisha mwili na ubongo wake vinapata nafasi ya kujirekebisha, kupumzika, na kujenga kinga dhidi ya maradhi.
Bingwa wa Magonjwa ya Ubongo na Mishipa ya Fahamu kutoka Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) – Mloganzila, Dk. Brighton Mushengezi, anasisitiza kuwa usingizi ni hitaji la msingi kama chakula au mazoezi.
"Usingizi ni sehemu ya afya. Husaidia kuzuia magonjwa ya moyo, kisukari, kuongeza kinga ya mwili na kupunguza msongo wa mawazo," anasema.
"Kama hujalala vya kutosha kwa siku kadhaa, unaweza kuwa na kile kinachoitwa 'deni la usingizi'. Hali hii huleta uchovu wa kudumu, kupoteza umakini, hasira, na hata matatizo ya kihisia.
FOLENI, PILIKAPILIKA
Uchunguzi uliofanywa na Nipashe umebaini kuwa wakazi wengi wa Dar es Salaam hulala chini ya saa tano kwa siku. Wanaamka mapema, wengine kuanzia saa 10 alfajiri, ili kuwahi kazini, hasa wanaoishi maeneo kama Mbagala, Ubungo au Tegeta.
Utafiti wa pamoja wa Benki ya Dunia (WB) na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) mwaka 2021 ulithibitisha kuwa kabla ya kuanzishwa kwa mradi wa Mabasi Yaendayo Haraka (BRT), wakazi walipoteza hadi saa tatu kila siku barabarani. Matokeo yake ni uchovu, afya duni ya akili na kupungua kwa ubora wa maisha.
MZIZI WA TATIZO
Daktari wa Afya ya Akili, Raymond Mgeni, anasema ukosefu wa usingizi huathiri moja kwa moja utendaji wa ubongo na afya ya akili.
Anaeleza kuwa watu wanaolala kwa saa chache huwa na dalili za kusahau vitu, hasira za mara kwa mara, kupungua kwa uwezo wa kufanya uamuzi, msongo wa mawazo, huzuni au hata dalili za sonona (depression).
"Kwa miji mikubwa, watu hushindwa kulala kutokana na presha ya kazi, hali ya maisha, na baadhi hufikia hatua ya kutegemea vilevi au dawa za usingizi ili kupata muda wa kupumzika," anasema Dk. Mgeni.
Vilevile, ameeleza kuwa baadhi ya watu wanatumia pombe au dawa za kulevya kama mbinu ya kupata usingizi, hali ambayo huongeza matatizo mengine ya kiafya na kiakili.
USINGIZI KWA UMRI
Dk. Mushengezi anaeleza kuwa mahitaji ya usingizi hutofautiana kulingana na umri: watoto wachanga wenye umri wa kuanzia miezi 0-3 wanahitaji kulala kwa saa 14-17 kwa siku na wenye umri wa kuanzia miezi 4-11 wanapaswa kulala kwa saa 12-15 kwa siku.
Anaelekeza kuwa wenye umri wa miaka 1-2 wanahitaji kulala kwa saa saa 11-14, miaka 6-13 wanahitaji kulala saa 9-11 kwa siku, miaka 14-17 wanatakiwa kupata saa 8-10 za kulala kila siku na watu wazima (miaka 18+) wanahitaji kulala kwa saa 7-9 kwa siku.
"Kutopata muda huu wa kulala husababisha mwili kushindwa kujirekebisha, hali inayoweka mazingira ya kupata magonjwa ya muda mrefu kama kisukari, presha, na hata saratani," Dk. Mushengezi anaonya.
MSAIKOLOJIA TIBA
Msaikolojia Tiba, Chris Mauki anachambua kwa kina faida za kisaikolojia za kulala. Anaeleza kuwa usingizi ni muda muhimu ambao ubongo hupumzika na kuandaa mfumo wa hisia na mantiki kwa siku inayofuata.
"Ubongo wa hisia unasaidia kuchambua matukio ya kihisia kama hasira, huzuni au furaha. Bila usingizi wa kutosha, mtu hupoteza uwezo wa kuchakata hisia hizi na matokeo yake ni kuongezeka kwa mhemko na msongo wa mawazo," anaeleza.
Mauki anaongeza kuwa binadamu anayekosa usingizi huwa na hali ya kuchoka, hasira, kupoteza umakini kazini na hata matatizo ya kijamii kama ugomvi katika familia au mahali pa kazi.
"Ni kama kompyuta inayofanya kazi bila kupumzika, lazima itaanza kufeli. Ndivyo ilivyo kwa ubongo wetu," Mauki anafafanua.