Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Tundu Lissu, amehoji ratiba ya Mahakama Kuu, Masjala Ndogo ya Dar es Salaam, baada ya kuonesha tarehe ya hukumu ya kesi ya uhaini inayomkabili, ilhali hadi sasa hakuna shahidi hata mmoja aliyesikilizwa.
Lissu aliwasilisha hoja tatu mbele ya jopo la majaji watatu likiongozwa na Jaji Dunstan Ndunguru, likisaidiwa na Majaji James Karayemaha na Ferdinand Kiwonde, akisema anahitaji ufafanuzi wa masuala hayo kabla ya usikilizwaji wa kesi kuendelea.
“Nipo tayari, lakini kabla hatujaanza nina mambo matatu ambayo naomba Mahakama inipatie maelezo. Septemba 30 mwaka huu, Naibu Msajili Livin Lyakinana aliniandikia barua kupitia kwa Mkuu wa Gereza la Ukonga, ambayo niliipokea Oktoba 2 mwaka huu,” amesema Lissu.
Ameeleza kuwa barua hiyo ilielekeza awasilishe orodha ya watu 100 anaowataka wahudhurie kesi hiyo, wakiwemo mawakili, viongozi wa chama, wanachama na ndugu zake, na kwamba majibu yake yafikishwe kwa Naibu Msajili kabla ya saa 12 jioni ya Oktoba 3 mwaka huu.
“Kwa kuwa nipo gerezani, sina mawasiliano na ndugu, mawakili wala viongozi, lakini nilijitahidi mwenyewe kuandaa orodha hiyo ndani ya muda,” amesema Lissu, akidai kuwa baadhi ya watu aliowataja walizuiwa kuingia mahakamani, akiwemo ndugu yake aliyesafiri kutoka Ujerumani.
“Leo nimeona ndugu yangu mwenyewe akizuiwa langoni. Kama mna orodha yangu, yeye ni namba 12. Amekuja kuona jinsi Mahakama za Tanzania zinavyotenda haki katika kesi hii ya uhaini,” amesema Lissu, akidai kuwa watu wengine pia walipigwa nje ya geti.
Amehoji: “Nataka kujua, hii ni Mahakama ya Polisi au Mahakama ya Tanzania? Nani anaamua nani aingie — Majaji, Polisi au wale wanaonishtaki kwa uhaini?”
Lissu amesema kama alielekezwa kuwasilisha majina na amefanya hivyo, basi haoni mantiki ya watu kuendelea kuzuiwa. “Hii ni Mahakama ya kisheria, siyo ya watu wasiojulikana. Naomba waliyozuiliwa waruhusiwe kuingia,” amesisitiza.
Akizungumzia hoja yake ya pili, Lissu amesema Oktoba 1 mwaka mhuu alipokea barua nyingine kutoka kwa Naibu Msajili iliyomtaka ahudhurie kikao cha maandalizi (pre-session meeting) kwa njia ya mtandao siku iliyofuata, Oktoba 3, saa nane mchana.
“Ofisa aliyeniletea barua hiyo nilimwambia airudishe kwa aliyemtuma. Naomba Mahakama inifafanulie hii pre-session meeting ni nini hasa?” amehoji.
Aidha, amesema barua hiyo iliambatana na nyaraka zilizotaja ratiba ya usikilizwaji wa kesi kuanzia Oktoba 6 hadi 24 mwaka huu kisha mapumziko ya siku 10, kabla ya kuendelea tena Novemba 3 hadi 11 mwaka huu — na Novemba 12 mwaka huu kuonesha kama tarehe ya hukumu.
“Leo ni Oktoba 6, hatujasikiliza hata shahidi mmoja. Hii hukumu inatoka wapi? Kama hukumu ipo, itolewe nijue moja — kama nanyongwa au la,” amesema Lissu.
Baada ya hoja hizo, jopo la majaji liliahirisha kesi hiyo kwa nusu saa ili kutoa ufafanuzi kuhusu masuala matatu yaliyowasilishwa na Lissu.