Tume ya Uchaguzi Zanzibar imefunga rasmi daftari la kudumu la wapiga kura

Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC), Jaji George Joseph Kazi, amesema tume hiyo imefunga rasmi daftari la kudumu la wapiga kura kama hatua muhimu ya maandalizi ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, mwaka huu.

Akizungumza katika Ofisi za ZEC Maisara leo, wakati wa warsha iliyowakutanisha waangalizi wa uchaguzi na waandishi wa habari kuhusu maandalizi ya uchaguzi, Jaji Kazi amesema jumla ya wapiga kura 717,557 wanatarajiwa kushiriki katika uchaguzi huo kupitia vituo 457 ambavyo vitajumuisha vituo vidogo vya kupigia kura 1,752 vilivyogawanywa katika majimbo 50 ya uchaguzi Zanzibar.

Kuhusu kura ya mapema, Mwenyekiti huyo amesema ZEC imetenga maeneo 50 ambapo kila jimbo litakuwa na kituo kimoja cha kupiga kura kwa ajili ya utaratibu huo.

Aidha, amewataka vyama vya siasa kuendelea kufanya kampeni kwa amani, kufuata sheria, kanuni na maadili ya uchaguzi, huku akipongeza mwenendo wa kampeni unaoendelea kwa ustaarabu.

Jaji Kazi amebainisha kuwa ZEC inaendelea na majukumu yake ya maandalizi ya uchaguzi, yakiwemo kuhamisha taarifa za wapiga kura na kuwaondoa wale waliopoteza sifa katika daftari la kudumu.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Uchaguzi wa ZEC, Thabit Idarous Faina, amesema kati ya wapiga kura 717,557 waliomo katika daftari hilo, wanawake ni 378,334 sawa na asilimia 53, na wanaume ni 339,223 sawa na asilimia 47.

Faina amesisitiza kuwa wadau wa uchaguzi ni kiungo muhimu katika mchakato wa kidemokrasia na wana nafasi kubwa ya kusaidia tume kufanikisha uchaguzi kwa mujibu wa sheria. Alisema miongoni mwa malengo ya uchaguzi huo ni kuhakikisha viongozi wa nchi wanapatikana kwa njia ya kidemokrasia na maamuzi ya wengi.

Aidha, amewataka waangalizi wa uchaguzi kuhakikisha kunakuwepo na uwazi na uadilifu, huku wakizingatia haki za wapiga kura, ili kusaidia kuepusha migogoro na kufuatilia kwa karibu mchakato mzima wa uchaguzi. Aliongeza kuwa wanapogundua kasoro au mafanikio, wanapaswa kuandika ripoti na kutoa mapendekezo yao kwa Tume ya Uchaguzi.

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii