Shirika la Posta Tanzania limetoa msaada wa vifaa mbalimbali vya wagonjwa katika Hospitali ya Ocean Road ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya Wiki ya Huduma kwa Wateja na kuelekea Siku ya Posta Duniani inayoadhimishwa kila mwaka Oktoba 9.
Akizungumza Oktoba 8 mwaka huu Meneja wa Posta Mkoa wa Dar es Salaam, Bw. Paul Mshanga kwa niaba ya Postamasta Mkuu ameeleza kuwa msaada huu ni sehemu ya kutambua mchango mkubwa wa jamii katika mafanikio ya Shirika na pia Shirika linaahidi kuendelea kutoa huduma zinazogusa maisha ya watu na kujikita katika kurudisha kwa jamii kama sehemu ya uwajibikaji kwa kijamii.
Aidha Shirika la Posta limetumia nafasi hiyo kuhamasisha matumizi ya huduma zake za kisasa na kidijitali ikiwemo Duka Mtandao Posta Kiganjani na huduma ya usafirishaji Swifpack ambazo zinatoa suluhisho la kisasa kwa mahitaji ya mawasiliano, biashara na malipo.
Akizungumza kwa niaba ya Hospitali, Bw. Malkiory Niniko, Meneja wa Huduma za Ustawi wa Jamii, ameishukuru Posta kwa msaada huo na kuguswa kwao na mahitaji ya wagonjwa.
Aidha amesisitiza umuhimu wa watumishi wa Posta kuchunguza afya zao mara kwa mara na kufungua milango ya ushirikiano zaidi kati ya hospitali ya Ocean Road na Shirika la Posta katika nyanja za kijamii na afya.
Hata hivyo msafara wa kukabidhi msaada huo uliongozwa na Meneja wa Posta Mkoa wa Dar es Salaam, Bw. Paul Mshanga kwa niaba ya Postamasta Mkuu huku akiambatana na Meneja wa Huduma za Posta Mkoa wa Dar es Salaam Bw. Khamis Swedi pamoja na maafisa waandamizi kutoka Makao Makuu ya Posta na ofisi ya Mkoa wa Dar es Salaam.