Tanzania kufanya majadiliana na Marekani kuhusu Viza

Serikali ya Tanzania imesema itafanya mazungumzo na Serikali ya Marekani kuhusiana na utaratibu uliowekwa kwa Tanzania na nchi zingine za Afrika kwenye orodha ya nchi ambazo raia wake watatakiwa kuweka dhamana ya viza kuingia nchini Marekani.

Katika taarifa iliyotolewa na kutiwa saini na Katibu Mkuu Wizara ya Habari Utamaduni Sanaa na Michezo na Msemaji Mkuu wa Serikali Gerson Msigwa imesema Tanzania imekuwa na uhusiano mzuri na Marekani kwa miongo minne.

“Pamoja na hatua ya Marekani kutangaza kuanzisha utaratibu wa dhamana na viza kwa raia wa Tanzania watakaoomba viza tajwa hapo juu , Serikali inapenda kuuhakikishia umma kwamba itaendelea na majadiliano hayo na Serikali ya Marekani kwa njia za kidiplomasia ili kutafuta suluhisho lenye kuzingatia usawa” imesema sehemu ya taarifa ya Serikali.

Kadhalika na hayo Serikali ya Tanzania inasisitiza kwamba uhusiano wake na Marekani umejengwa katika misingi ya urafiki ushirikiano na kuheshimiana kwa muda mrefu na hivyo haitabadilisha dhamira ya Tanzania ya kuendeleza  uhusiano mzuri na nchi hiyo kwa manufaa ya pande zote.

 Kwa mujibu wa taarifa ya Marekani raia wa nchi hizo ikiwemo Tanzania ambaye atastahiki viza ni lazima atume bondi ya dola 5000 za kimarekani, dola 10,000 au 15,000. 

 “Kiasi kinatambuliwa wakati wa mahojiano ya visa.  Mwombaji lazima pia awasilishe Idara ya Usalama wa Nchi Fomu I-352.  Ni lazima waombaji wakubali masharti ya dhamana, kupitia jukwaa la malipo la mtandaoni la hazina.”  

 “Dhamana haitoi dhamana ya utoaji wa visa.  Ikiwa mtu analipa ada bila maelekezo ya ofisa wa kibalozi, mtu huyu hatarejeshewa pesa hizo.”imesema sehemu ya taarifa ya Marekani.

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii