Mgombea urais wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. Samia Suluhu Hassan amesema ujenzi wa soko la Lamadi wilayani Busega mkoani Simiyu umechelewa kutokana na mvutano wa viongozi wa halmashauri kuhusu eneo la kujenga mradi huo licha ya fedha tayari kutengwa.
Akizungumza leo Oktoba 9 mwaka huu katika mkutano wa kampeni uliofanyika Lamadi Dk. Samia amesema ahadi hiyo aliitoa kwa wananchi wa Lamadi na kwamba serikali imetenga fedha kwa ajili ya utekelezaji wake lakini mvutano wa mahali pa kujenga kati ya Lamadi na Nyashimo umezuia utekelezaji huo.
Amebainisha kuwa ahadi yake ya soko ni kwa ajili ya wananchi wa Lamadi huku akifafanua kuwa Nyashimo ilipangiwa kupata stendi ya mabasi kama mradi tofauti.
Hata hivyo Samia yupo mkoani Simiyu kwa ziara ya kampeni za uchaguzi ambapo ameanza mikutano yake Lamadi kabla ya kuelekea Busega na baadaye kuendelea na kampeni mkoani Mara katika maeneo ya Bunda na Musoma Mjini.