Uwekezaji wa Serikali wafikia trilioni 92.3

Uwekezaji uliofanywa na serikali ndani na nje ya nchi umeongezeka kwa asilimia 7 hadi kufikia Sh92.29 trilioni Juni 30 mwaka huu kutoka Sh86.3 trilioni katika mwaka wa fedha 2023/24.

Uwekezaji huo wa serikali unahusisha mashirika ya umma 255 na kampuni 45 ambayo serikali ina umiliki wa hisa chache na taasisi za kigeni 10 zote kwa pamoja zinatengeneza uti wa mgongo wa mapato yasiyo ya kodi ya Tanzania. 

Katika kipindi cha miaka mitano uwekezaji wa ndani umeongezeka kutoka Sh67.01 trilioni mwaka 2020/21 hadi Sh90.61 trilioni mwaka 2024/25 jambo linalodhihirisha utendaji bora na usimamizi ulioboreshwa katika mashirika ya umma.

Jambo hili limeenda sambamba na kukua kwa thamani ya uwekezaji wa serikali katika taasisi za nje ambao ulitoka Sh722.94 bilioni hadi Sh1.68 trilioni.

Takwimu hizi zinazopatikana kwenye Taarifa ya Msajili wa Hazina ya mwaka ulioishia Juni 30 mwaka huu zinaeleza kuwa ukuaji huo umetokana na utendaji bora wa mashirika muhimu ya umma na ufanisi katika uendeshaji wa taasisi mbalimbali.

Msajili wa Hazina Bw Nehemiah Mchechu alisema ongezeko hilo linaonyesha juhudi endelevu za serikali katika kuimarisha usimamizi na utawala bora wa uwekezaji wa umma.

“Ukuaji huu wa uwekezaji unaonesha maboresho katika utawala wa mashirika umma, uhusiano wake na malengo ya maendeleo ya taifa,” alisema Bw Mchechu.

Kwa mujibu wake mashirika makubwa kadhaa yamechangia kwa kiasi kikubwa katika ongezeko la mtaji wa serikali.

Kwa mfano Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) ulirekodi ongezeko la asilimia 29 katika mali halisi, kutoka Sh7.2 trilioni hadi Sh9.3 trilioni.

Kichocheo kikubwa ni uandikishaji wa wanachama wapya kutoka sekta isiyo rasmi na ujumuishaji na mifumo mingine ya serikali kama Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA) na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).

Sanjari na NSSF Mfuko wa Pensheni kwa Watumishi wa Umma (PSSSF) ulionesha ongezeko la asilimia 13 katika mali halisi, kutoka Sh8.12 trilioni hadi Sh9.2 trilioni.

Ukuaji huu ulichochewa zaidi na kuongezeka kwa michango ya wanachama kufuatia ajira mpya na vyeo kwa watumishi wa umma.

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii