Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi Vijana Ajira na Wenye Ulemavu Bi. Mary Maganga,ametembelea mabanda ya vijana katika Maadhimisho ya Wiki ya Vijana Kitaifa na kufurahishwa na ubunifu unaooneshwa na vijana.
Maganga amesema kuwa ubunifu huo unaonesha namna vijana walivyo na uwezo wa kutumia maarifa na teknolojia katika kutatua changamoto zinazowakabili ndani jamii zao.
Aidha Maganga amepongeza kazi zinazotekelezwa na kundi la Watu Wenye Ulemavu ikiwemo ushonaji, matumizi ya TEHAMA pamoja na shughuli za ujasiriamali zinazochangia katika kujiajiri na kukuza uchumi wa mtu mmoja mmoja.
Hata hivyo ameongeza kuwa Serikali itaendelea kuweka mazingira wezeshi kwa vijana na Watu Wenye Ulemavu ili waweze kutumia ujuzi wao kwa tija kupitia programu ya mikopo inayotolewa na Serikali.
“Ubunifu ni chachu ya maendeleo na unapaswa kuendelezwa katika sekta zote za uzalishaji,” amesema Bi. Maganga.