Mkurugenzi wa Mashtaka, Bw. Sylvester Mwakitalu amewataka wafanyakazi wa Ofisi ya Taifa ya Mashtaka kudumisha nidhamu kwa kufuata taratibu kanuni na miongozo ya utumishi wa umma katika utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku.
Mkurugenzi Mwakitalu ametoa wito huo wakati wa kikao na wafanyakazi wa Makao Makuu na Ofisi ya Mkoa wa Dodoma kilichofanyika Oktoba 8 mwaka huu katika jengo jipya la Makao Makuu ya Ofisi ya Taifa ya Mashtaka lililopo Kata ya Njedengwa Jijini Dodoma.
“Bado niendelee kusisitiza kuhusu nidhamu Ofisi ya Taifa ya Mashtaka ni taasisi inayounganisha ofisi nyingine kwa kuwa ndiyo nguzo ya mfumo wa haki jinai.
Hivyo tunapaswa kuwa wa kwanza katika nidhamu kwenye kila eneo iwe katika utekelezaji wa majukumu yetu au kuzingatia taratibu zinazoongoza watumishi wa umma na ofisi yetu .
Aidha Kikao hicho ni sehemu ya mfululizo wa vikao vya kila robo mwaka ambavyo hutoa fursa kwa Mkurugenzi wa Mashtaka kuzungumza na wafanyakazi kusikiliza changamoto wanazokutana nazo na kupokea mapendekezo ya kuboresha utendaji kazi ndani ya Ofisi ya Taifa ya Mashtaka.
Hivyo DPP Mwakitalu aliwaasa wafanyakazi kutunza miundombinu ya jengo jipya akisisitiza umuhimu wa kuhakikisha mali za serikali zinahifadhiwa vizuri kwa manufaa ya umma.
“Tumepata jengo zuri kubwa na lenye nafasi ya kutosha ukilinganisha na lile la awali lililokuwa dogo Ni wajibu wetu kulitunza na kuhakikisha hakuna uharibifu wa aina yoyote Kuwepo kwa miundombinu bora kutaimarisha utoaji wa huduma bora za kimashtaka kwa wananchi,” aliongeza DPP.
Ikumbukwe kuwa Makao Makuu ya Ofisi ya Taifa ya Mashtaka pamoja na Ofisi ya Mkoa wa Dodoma sasa zimehamia katika jengo jipya lililopo Mtaa wa Mashtaka Njedengwa karibu na Ofisi za Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi Jijini Dodoma ambapo awali ofisi hizo zilikuwa ndani ya Chuo Kikuu cha Dodoma.