Jeshi la Polisi Mkoa wa Dodoma linamshikilia kijana aitwaye Piere Saimoni (20) mkazi wa Nzuguni B kwa tuhuma za kujihusisha na vitendo vya ubakaji.
Kijana huyo anatuhumiwa kuwabaka wanawake wanne wa Mtaa wa Nzuguni B Oktoba 5 mwaka huu.
Baada ya kutokea tukio hilo, Polisi na wananchi wa mtaa huo walifanikiwa kumkamata mtuhumiwa baada ya kufanyika msako maalumu.
Inadaiwa kuwa mtuhumiwa huyo alikuwa akitumia mbinu ya kuingia kwa siri katika nyumba anamoishi mwanamke anayemlenga na kutekeleza kitendo hicho kwa kutumia vitisho vya kujeruhi.
Katika uchunguzi wa awali uliofanywa na Jeshi la Polisi, imebainika kuwa mtuhumiwa huyo anaishi katika nyumba moja na watu wengine 13. Mtuhumiwa atafikishwa mahakamani mara tu taratibu za kisheria zitakapokamilika.
Polisi Mkoa wa Dodoma inatoa wito kwa wananchi kuendelea kushirikiana na vyombo vya dola kwa kutoa taarifa za uhalifu na wahalifu pamoja na kuacha tabia ya kujichukulia sheria mikononi ili kudumisha amani na usalama katika jamii.