Serikali kupitia Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS) inaendelea na utekelezaji wa ujenzi wa miradi 13 ya dharura katika mkoa wa Lindi ambayo itatumia jumla ya shilingi Bilioni 119 kwa ajili ya kukamilisha ujenzi wa miradi hiyo ya dharura.
Akizungumza mara baada ya kutembelea na kukagua hatua zilizofikiwa za ujenzi wa miradi hiyo Msimamizi wa kitengo cha Miradi ya Maendeleo TANROADS Mkoa wa Lindi Mhandisi Fred Sanga amesema kuwa mpaka sasa jumla ya shilingi Bilioni 58.5 zimeshalipwa kwa mkandarasi na inatarajiwa kukamilika Disemba mwaka huu.
Miradi hiyo ni pamoja na Ujenzi wa Daraja la Kipwata (Mita 40) na Boksi kalavati eneo la Sakura na Songas, Ujenzi wa Daraja la Mikereng’ende (mita 40) na Boksi kalavati katika maeneo ya Mtandango/Stakishari na Masaninga, Ujenzi wa Boksi kalavati la Mbwemkuru I (seli 4, 5m x 4m), na matuta ya kuzuia mmomomnyoko wa udongo ( Spur dykes), Ujenzi wa Daraja la Somanga Mtama (60m) na Ujenzi wa Daraja la Njenga II (60m) ambapo miradi yote hii ipo katika barabara Kuu ya Marendego – Lindi – Mingoyo
Aidha Mhandisi Sanga amesema kuwa katika mwaka wa fedha 2025/2026 serikali imepanga kutumia Bilioni 16.2 kwa ajili ya Miradi ya Matengezo (Maintenance) kwa gharama ya Shilingi bilioni 13.3 huku Miradi ya Maendeleo (Development) ikitarajiwa kutumia shilingi Bilioni 2.9 kwa ajili ya ujenzi wa kilomita 405.15 za barabara za lami sambamba na ujenzi wa kilomita 901.54 za barabara za Changarawe.
Miradi mingine ni Ujenzi wa Daraja la Miguruwe (39m) pamoja na Boksi kalavati nne (4), Ujenzi wa Daraja la Zinga (18m) na Ujenzi wa Daraja la Kimambi (39m) ambayo ipo katika Barabara ya Mkoa ya Nangurukuru – Liwale.
Kuanzia Oktoba 2023 hadi kufikia Mei, 2024 Tanzania ilikumbwa na kadhia ya mvua kubwa zilizotawala zikichangiwa na tukio la asili la hali ya hewa El-Nino pamoja na Kimbunga Hidaya lililoathiri hali ya hewa nchini na kusababisha athari hasi kwa wananchi kukosa makazi, vifo, magonjwa ya milipuko, uharibifu wa miundombinu ya barabara pamoja na madaraja.