Mwenyekiti wa chama cha Demokrasia na Maendeleo CHADEMA Tundu Lissu amepandishwa kizimbani asubuhi hii ya leo Oktoba 13 mwaka huu katika Mahakama Kuu ya Tanzania Masijala Ndogo ya Dar es salaam kwa ajili ya muendelezo wa ushahidi katika kesi yake ya uhaini.
Ambapo leo Mahakama hiyo inatarajiwa kutoa uamuzi mdogo wa pingamizi lililoibuliwa na upande wa Jamhuri juu ya maelezo ya Shahidi yaliyoombwa na Lissu ya kutaka yapokelewe na mahakama ili kuyatumie katika maswali ya dodoso.
Ikumbukwe kuwa Lissu anakabiliwa na kesi ya uhaini ambayo ipo katika hatua ya usikilizwaji huku akidaiwa kutenda kosa hilo Aprili 10 mwaka huu jijini Dar es salaam ambapo uamuzi huo mdogo utatolewa na Jopo la Majaji watatu wakiongozwa na Jaji Dunstan Ndunguru akisaidizana na Jaji James Karayemaha na Ferdinand Kiwonde.
Awali Lissu alianza kwa kuuliza maswali ya dodoso kwa shahidi ambaye ni Mkaguzi wa Polisi kutoka katika Kitengo cha Upelelezi wa Makosa ya Mtandao, PF22863 John Kaaya(45) baada ya jamhuri kuhitimisha ushahidi wa msingi.