Zoezi la kura ya mapema limeanza kwa mafanikio makubwa visiwani Zanzibar, likiendelea katika hali ya amani, utulivu na uwazi, huku Wapiga Kura wenye sifa za Kupiga Kura hiyo, wakijitokeza kutekeleza haki yao ya kikatiba ya Kupiga Kura.
Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC), Mhe.Jaji George J. Kazi, amesema kuwa , Tume imeridhishwa na mwenendo wa zoezi hilo ambalo limefanyika kwa wakati na maandalizi bora katika vituo vyote 50 vya kupigia kura vilivyopangwa.
Akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kufanya ziara katika baadhi ya vituo vya kupigia kura, Jaji Kazi alisema, mwitikio wa Wapiga Kura umekuwa mzuri na utaratibu wa Upigaji Kura umefuatwa kwa mujibu wa kanuni na taratibu za Tume.
Alifafanua kuwa Kura ya Mapema ni sehemu muhimu ya mchakato wa Uchaguzi Mkuu wa Zanzibar, inayolenga kutoa fursa kwa makundi maalum ambayo siku ya Uchaguzi Mkuu yatakuwa na majukumu mengine ya Kiuchaguzi,
Ameongeza kuwa wale waliokuwa na sifa ya kupiga Kura ya Mapema lakini hawakupata fursa siku ya leo, wataruhusiwa Kupiga Kura kesho endapo watakuwa wamepata nafasi.
Mwenyekiti huyo wa Tume ametoa wito kwa wananchi wote wa Zanzibar kujitokeza kwa wingi siku ya leo Oktoba 29 mwaka huu kushiriki katika Uchaguzi Mkuu kwa amani, akisisitiza kuwa kufanya hivyo ni kutimiza wajibu wa kikatiba na kulinda demokrasia ya nchi.