Menejimenti ya Wizara ya Madini Oktoba 27 mwaka huuu ilikutana na Wakuu wa Taasisi zake katika kikao kilicholenga kupokea taarifa ya ufuatiliaji na tathmini kwa majukumu yaliyotekelezwa na taasisi hizo katika kipindi cha Robo ya Kwanza ya Mwaka wa Fedha 2025/26.
Taasisi zilizo chini ya Wizara ni pamoja na Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST) Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) Tume ya Madini Taasisi ya Uhamasishaji Uwazi na Uwajibikaji katika Rasilimali Madini Mafuta na Gesi Asilia (TEITI) na Kituo cha Jemolojia Tanzania (TGC) cha jijini Arusha.
Katika taarifa iliyowasilishwa na Tume ya Madini ilielezwa kwamba katika kipindi robo ya kwanza tayari kiasi cha shilingi bilioni 315.4 kimekusanywa ikiwa ni sawa na asilimia 105.14 ya lengo la kukusanya shilingi 299.98 bilioni katika robo hiyo Katika mwaka wa fedha 2025/26 Wizara imepangiwa kukusanya shilingi trilioni 1.4.
Kwa upande wa STAMICO pamoja na mambo mengine taarifa ilieleza kuwa zoezi la kusimika mitambo ya uzalishaji wa mkaa wa Rafiki Briquettes unaotokana na makaa ya mawe unaozalishwa na shirika hilo hivi karibuni itasimikwa katika mikoa ya Dodoma na Tabora.
Tayari mitambo kama hiyo inaendelea na uzalishaji wa nishati hiyo jijini Dar es Salaam katika eneo la Kisarawe, Pwani na Kiwira mkoani Songwe.
Aidh shirika hilo lilisistiza kuhusu azma yake ya kuendeleza leseni zake za madini muhimu na mkakati zilizopo katika maeneo mbalimbali nchini ikiwa ni hatua ya kulifanya kuingia katika uwekezaji mkubwa.
Vilevile ilielezwa kuwa katika robo ya kwanza ya mwaka 2025/26 jumla ya kilo2,356.413 zimesafishwa katika Kiwanda cha Kusafisha Dhahabu cha Mwanza Precious Metals Refinery chenye ubia na STAMICO kwa ajili ya Banki Kuu ya Tanzania.
Hata hivyo ilielezwa kwamba hadi sasa kiasi cha tani 12 za dhahabu tayari zimenunuliwa na BoT.