Mhe,Chumi awahakikishia waangalizi uchaguzi huru

Serikali imeihakikishia Timu ya Waangalizi ya Uchaguzi ya Wabunge-Wanawake kutoka Jumuiya ya Madola (CWP) kuwa Uchaguzi Mkuu wa Rais, wabunge na madiwani uliopangwa kufanyika Oktoba 29 mwaka huu utakuwa huru, haki na wazi.

Kauli hiyo imetolewa na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Cosato Chumi alipokutana na timu hiyo jijini Dodoma Oktoba 28 mwaka huu.

Mhe. Chumi alisema Serikali kupitia taasisi husika zikiwemo Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) na Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC), imekamilisha maandalizi yote muhimu kuhakikisha kuwa uchaguzi huo unafanyika kwa kuzingatia Katiba ya Nchi, sheria za uchaguzi na vigezo vya kidemokrasia. 

Alisema kuwa uchaguzi wa mwaka huu ni wa aina yake kutokana na kuwa jumuishi zaidi ambapo wagombea 17 wa nafasi ya Rais watatu ni wanawake na 10 ni wagombea mwenza, huku ikishuhudiwa pia kuwa idadi kubwa ya wanawake wanawania nafasi za ubunge na udiwani katika pande zote za muungano.

Naye Kiongozi wa timu hiyo Mhe. Ndangiza ameeleza kuwa timu yake tangu ilipowasili nchini, imekutana na wawakilishi mbalimbali wa Serikali wakiwemo INEC na kutembelea baadhi ya vituo vya kupigia kura jijini Dodoma na kuridhishwa na maandalizi yaliyofanywa.

Aidha, timu hiyo imefurahishwa na uamuzi wa vyama vya siasa nchini kuteua idadi kubwa ya wanawake kuwania nafasi mbalimbali za uongozi na kuahidi kuwa uangalizi wao wa uchaguzi nchini, utazingatia miongozo ya misheni za kimataifa za uchaguzi. 

Wamekamilisha mazungumzo yao kwa kutoa wito kwa nchi za Afrika kuiga mfano wa Tanzania kwa kuendesha kampeni na baadaye uchaguzi kwa amani na utulivu, kwa kusisitiza kuwa uchaguzi sio vita.

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii