Kesi namba 26287/2025 ya iliyofunguliwa dhidi ya Mkuu wa Jeshi la Polisi Nchini(IGP) na wenzake imeahirishwa mpaka jumatatu ya novemba 10 mwaka huu.
Kesi hiyo imeitwa kwa mara ya kwanza leo Novemba 7 mwaka huu katika Mahakama Kuu ya Tanzania Masjala Ndogo ya Dar es Salaam mbele ya Jaji Bwegoge ambapo upande wa mlalamikaji(Heche) uliieleza mahakama kuwa walalamikiwa wanapaswa kumfikisha mahakamani mteja wao haraka kwani anashikiliwa takribani wiki tatu na Jeshi la Polisi bila kushtakiwa ikiwa ni kinyume na sheria.
Wakili Mwandamizi Mpale Mpoki aliieleza mahakama kuwa wanaomshikilia mteja wao kama wanadhani ana makosa basi wamfikishe mbele ya mahakama na kumshtaki kwa mujibu wa sheria.
Upande wa Jamhuri ulieleza mahakama kuwa unahitaji muda ili kuweza kuandaa na kuwasilisha kiapo kinzani hivyo wapate muda.
Hata hivyo Wakili Mpoki aliieleza mahakama kuwa kwa kujali uhuru na haki za mteja wake aliyekamatwa Oktoba 22 mwaka huu ni vyema mahakama ikazingatia maombi yao.
Hivyo kesi hiyo imeahirishwa mpaka jumatatu ya Novemba 10 mwaka huu saa nne na nusu ili kutoa nafasi kwa upande wa Jamhuri kuandaa kiapo kinzani ambacho wameamrishwa ifikapo jumapili ya Novemba 09 mwaka huu kiwe kimewasilishwa katika mfumo wa Mahakama.