Jumla ya wanafunzi 29,193 wanatarajiwa kufanya Mtihani wa Upimaji wa Kidato cha Pili mkoani Shinyanga, ambao unatarajiwa kuanza rasmi Novemba 10 hadi 19 katika shule mbalimbali za sekondari mkoani humo.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo na Afisa Elimu wa Mkoa wa Shinyanga, Samson Hango amesema kati ya wanafunzi hao, wavulana ni 12,103 na wasichana ni 17,090, huku watahiniwa 42 wakiwa ni wenye mahitaji maalumu.
Aidha Hango amewahimiza wazazi na walezi kuhakikisha wanafunzi wote waliojiandikisha wanafika kwenye vituo vyao vya mtihani kwa wakati ili kutimiza wajibu wao wa msingi wa kitaaluma.
"Ni muhimu wazazi na walezi wakawapa wanafunzi motisha na kuhakikisha wanatimiza wajibu wao kwa kufanya mtihani huu kwa utulivu, kwani ni hatua muhimu katika maendeleo yao ya elimu," amesema Hango.
Hata hivyo ametoa onyo kali kwa walimu watakaobainika kuhusika katika vitendo vya udanganyifu wa mitihani au kukwamisha zoezi hilo kwa namna yoyote ile, na kwamba mtihani huo ni wa upimaji wa kawaida.