Mfuko wa Misitu Tanzania (TaFF) umetoa zaidi ya sh.milioni 130 kuviwezesha zaidi ya vikundi 13 vya ufugaji nyuki vilivyopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Kigoma ili kuboresha kipato cha wananchi na kuimarisha uhifadhi wa rasilimali za misitu.
Kaimu Mtendaji Mkuu wa TaFF Dkt. Tuli Msuya ameeleza hayo wakati wa mafunzo kuhusu uandaaji wa taarifa za matumizi ya fedha za ruzuku kwa wanufaika wa miradi hiyo.
Amesisitiza kuwa ruzuku hizo ni mali ya wanavikundi wote na zinapaswa kutumika kwa uwazi umoja na uwajibikaji.
“Ruzuku iliyotolewa ni kwa manufaa ya wanavikundi wote, kwani kila mwanakikundi alishiriki kusaini andiko la mradi uliopatiwa ruzuku. Kila mmoja ana haki ya kujua kiasi cha fedha kilichopokelewa na kuhakikisha zinatumika kama zilivyokusudiwa,” amesema Dkt. Tuli.
Ameongeza kuwa vikundi vinapaswa kuhakikisha uendelevu wa miradi yao hata baada ya kumalizika kwa kipindi cha ruzuku, sambamba na kuzingatia masharti yaliyowekwa katika mkataba wa utoaji ruzuku uliosainiwa kati ya TaFF na wanufaika.
Kwa upande wake Mratibu wa Pathfinder Women Group (PFWG) Agnes Kayombo ameishukuru Wizara ya Maliasili na Utalii kupitia TaFF kwa kutoa ruzuku ya sh.milioni 10 kwa kikundi chao ambazo zimewawezesha kununua mizinga, mavazi ya kujikinga na vifaa vya kisasa vya ufugaji nyuki.
“Mpaka sasa tumeanza kuvuna matunda ya mradi wetu tumefanikiwa kulina zaidi ya lita 80 za asali ambazo tayari tumeuza Tunaishukuru sana TaFF kwa kutuamini na kutuwezesha. Wanawake tunapaswa kuona hii kama fursa ya kujikwamua kiuchumi,” amesema.
Ameongeza kuwa wanawake ni nguvu kubwa katika jamii na wana uwezo wa kufanikisha miradi ya maendeleo endapo watapata msaada na ufuatiliaji kama uliofanywa na TaFF.
Dkt. Tuli ameahidi kuwa TaFF itaendelea kushirikiana na vikundi vya wananchi katika sekta ya misitu na ufugaji nyuki, ili kuhakikisha jamii inanufaika kiuchumi huku ikihifadhi mazingira endelevu.