Mkuu wa Mkoa wa Mara Kanali Evans Mtambi ameagiza wilaya za Tarime na Rorya kulipisha jengo linalomilikiwa na Chama Kikuu cha Wakulima wa Mara (WAMACU) ndani ya muda wa mwezi mmoja, ili liweze kutumika kwa shughuli za uzalishaji katika sekta ya kilimo pamoja na ofisi za ushirika huo.
Agizo hilo limetolewa kufuatia malalamiko yaliyowasilishwa na wanachama wa WAMACU wakati wa ufunguzi wa Mkutano Mkuu wa 16 wa chama hicho uliofanyika mkoani humo.
Katika hatua hiyo wanachama hao walilalamikia hatua ya Jeshi la Polisi kukataa kurejesha jengo hilo, licha ya kwamba walikuwa wametoa kwa matumizi ya muda wakati wakijiandaa kujenga ofisi zao.
Hivyo kutokana na malalamiko hayo, Mkuu wa Mkoa alitoa maelekezo ya moja kwa moja kwa Jeshi la Polisi kuhakikisha linapisha jengo hilo haraka iwezekanavyo, ili kuwezesha shughuli za uzalishaji na maendeleo ya wakulima kuendelea bila vikwazo.
Aidha wanachama na viongozi wa WAMACU wameelezea kufurahishwa kwao na uamuzi huo, wakisema kurejeshwa kwa jengo hilo kutachangia kuimarika kwa shughuli za kiuchumi za wakulima, kuongeza tija katika sekta ya kilimo, na kukuza uchumi wa wananchi pamoja na taifa kwa ujumla.
#10YrsJembefm #Familiamoja #AhsantekwaTime