Mkuu wa Misheni ya Uangalizi wa Uchaguzi Mkuu wa Tanzania ya Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC-SEOM) ambaye pia ni Spika wa Mstaafu wa Bunge la Jamhuri ya Malawi Mhe. Richard Msowoya, amezindua rasmi Misheni hiyo katika hafla iliyofanyika jijini Dar es Salaam.
Akizungumza wakati wa uzinduzi huo Mhe. Msowoya amesema SADC inashiriki mchakato wa kidemokrasia wa uangalizi wa uchaguzi wa Tanzania kwa mwaliko wa Serikali, huku akiahidi kuzingatia maadili ya ufuatiliaji na tathmini, kuhakikisha chaguzi zinafanyika kwa viwango vya kimataifa na miongozo ya kikanda, na unakuwa huru na wa haki.
“Huu ni uchaguzi mkuu wa tatu ndani ya mwezi mmoja katika Kanda hii ya SADC ukifuata uchaguzi wa amani uliofanyika Malawi na katika visiwa vya Ushelisheli,” amesema Mhe. Msowoya huku akisisitiza umuhimu wa mshikamano wa kikanda katika kuimarisha misingi ya demokrasia.
Mhe. Msowoya ameeleza kuwa tangu ujumbe wa SEOM ulipowasili nchini umebaini kuwa licha ya kuendelea kwa shughuli za kampeni za uchaguzi kutoka kwa vyama mbalimbali vya siasa, nchi imeendelea kudumisha amani na utulivu, jambo linaloashiria kwamba Tanzania imekomaa katika kuimarisha na kutekeleza misingi ya demokrasia.
Ametaja vigezo muhimu vitakavyotumika kutathmini mwenendo wa uchaguzi mkuu nchini kuwa ni ushiriki wa raia katika mchakato wa kidemokrasia, uhuru na haki za binadamu, usawa wa vyama vya siasa katika kupata fursa kwenye vyombo vya habari, na hatua za kuzuia vurugu, vitisho na upendeleo wa kisiasa.
Vigezo vingine ni uadilifu wa taasisi za uchaguzi na mfumo wa sheria, elimu ya uraia na mpiga kura, haki ya kugombea na kupiga kura kwa uhuru, na umuhimu wa kukubali na kuheshimu matokeo ya uchaguzi.
Naye Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Said Shaib Mussa ameeleza kuwa, “Ushiriki wa waangalizi hawa unasaidia kukuza uwazi, usawa na haki katika mchakato wa uchaguzi, na hivyo kuimarisha demokrasia ya kweli katika nchi wanachama wa SADC ikiwemo Tanzania.”
Ujumbe wa Misheni ya SADC-SEOM nchini unajumuisha watu 80 kutoka nchi 10 wanachama wa SADC.