Serikali ya Ukraine imeripoti kuwa raia 1,436 kutoka Nchi 36 Barani Afrika wamejiunga na jeshi la Urusi katika vita dhidi ya Ukraine, huku ikionya kuwa idadi halisi huenda ni kubwa zaidi.
Kwa mujibu wa taarifa ya Waziri wa Mambo ya Nje wa Ukraine, Andriy Sybiha aliyoiandika Novemba 7 mwaka huu kupitia ukurasa wake wa X, amesema Urusi inawashawishi Waafrika katika mikataba ya kijeshi ambayo aliifananisha na “hukumu ya kifo,” kwa maelezo kuwa wengi wao hutumwa moja kwa moja kwenye mashambulizi hatari na kuuawa haraka.
Kwa mujibu wa taarifa ya Novemba 6 mwaka huu iliyochapishwa na Independent Online news (IOL news) kutoka Afrika Kusini, Serikali ya Taifa hilo ilisema inachunguza kuhusu Wanaume 17 wa Taifa hilo waliokwama Ukraine baada ya kilichosemwa ni “kudanganywa na mikataba ya ajira”.
Serikali ya Afrika Kusini ilitoa tahadhari kwa Wanawake Vijana kuhusu matangazo ya uongo yanayosambazwa na watu maarufu wa Mitandaoni, wakiahidi ajira na masomo nchini Urusi, kufuatia visa vya udanganyifu vilivyogunduliwa mwaka uliopita.
Oktoba 27 mwaka huu chombo cha Habari nchini Kenya cha Citizen Digital kiliandika kuwa baadhi ya raia wa Kenya walikamatwa katika kambi za Kijeshi nchini Urusi baada ya kujikuta kwenye mgogoro bila kujua ikionesha jinsi raia wa Afrika wanavyodanganywa kuingia vitani huku juhudi za kidiplomasia zikifanyika ili kuwaondoa.
Taarifa ya chombo hicho ilieleza kuwa “Serikali imethibitisha kuwa inaendeleza juhudi za kidiplomasia kuhakikisha kuachiliwa na kurejea salama kwa Wakenya waliokwama katika operesheni za kijeshi za Urusi”.
Aidha taarifa ya Sybiha imesema "kuna njia mbili za kuepuka hatima kama hiyo. Kwanza, msijiunge na jeshi la Urusi wala msisaini hati yoyote na mamlaka za Urusi. Natoa wito kwa serikali zote za Nchi za Afrika kuwaonya raia wao hadharani dhidi ya kujiunga na jeshi la uvamizi la Urusi,”.