DALALI WA MAHAKAMA ASHIKILIWA KWA TUHUMA ZA WIZI WA KUAMINIWA

Jeshi la Polisi Mkoa wa Geita linamshikilia Wema Haibe (38), Dalali wa Mahakama, kwa tuhuma za wizi wa kuaminiwa baada ya kuuza nyumba aliyokabidhiwa na Mahakama kisha kuiba fedha milioni 22.

Mtuhumiwa akiwa mwenye dhamana ya utekelezaji wa amri ya Mahakama ya Mwanzo Wilaya ya Geita – Kituo cha Nyankumbu, iliyotolewa kufuatia Shauri la Talaka Na. 65/2024, alielekezwa kuuza kwa mnada nyumba ya wanandoa Joseph Kalinda na Ndimira Kasisi iliyopo maeneo ya Fadhili Bucha, Kata ya Buhalahala, Wilaya ya Geita na kutakiwa kuweka fedha kwenye akaunti ya Mahakama ambalo ni takwa la kisheria.

Hata hivyo, mnamo Aprili 4 huu mtuhumiwa aliuza nyumba hiyo kwa Tatizo Balanzila (56) kwa kiasi cha Shilingi Milioni 22 (22,000,000/=). Kinyume na maelekezo ya Mahakama, mtuhumiwa aliweka fedha hizo kwenda kwenye akaunti yake binafsi badala ya akaunti ya Mahakama kama alivyoagizwa.

Jeshi la Polisi linaendelea na uchunguzi wa kina, na mtuhumiwa atafikishwa Mahakamani mara baada ya taratibu zote za kisheria kukamilika.

Jeshi la Polisi litaendelea kuchukua hatua kwa mujibu wa sheria, na linawataka wananchi pamoja na madalali wanaotekeleza amri za Mahakama kuhakikisha wanatekeleza majukumu yao kwa uadilifu, uaminifu na kufuata taratibu za kisheria.

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii