Juisi ya karoti ni kinywaji chenye virutubisho vingi muhimu kama vitamini, antioxidants na nyuzinyuzi, ambavyo huchangia kuboresha afya kwa ujumla hivyo kwa mujibu wa Healthline, juisi ya karoti ina kalori chache na wanga mdogo lakini ina virutubisho muhimu kwa mwili.
Kikombe kimoja (takriban gramu 236) cha juisi ya karoti kina wastani wa:
Kalori 94
Protini gramu 2
Mafuta chini ya gramu 1
Wanga gramu 22
Sukari gramu 9
Nyuzinyuzi gramu 2
Pia hutoa:
251% ya mahitaji ya kila siku (DV) ya vitamini A
22% ya DV ya vitamini C
31% ya DV ya vitamini K
15% ya DV ya potasiamu
Karoti zina carotenoids kama lutein na zeaxanthin ambazo hufanya kazi kama antioxidants, pamoja na beta carotene inayobadilishwa na mwili kuwa vitamini A.
Hizi hapa ni faida 7 za juisi ya karoti:
1. Huboresha afya ya macho
Juisi ya karoti ina vitamini A kwa wingi, ambayo ni muhimu kwa kuona vizuri. Ulaji wa vyakula vyenye provitamin A umehusishwa na kupunguza hatari ya upofu na magonjwa ya macho yanayohusiana na uzee.
Lutein na zeaxanthin hulinda macho dhidi ya mwanga hatarishi na hupunguza hatari ya macular degeneration.
2. Huimarisha kinga ya mwili
Juisi ya karoti ina vitamini A, C na B6 ambazo husaidia kuimarisha kinga ya mwili. Vitamini B6 ni muhimu kwa utendaji mzuri wa kinga, na upungufu wake unaweza kudhoofisha uwezo wa mwili kupambana na magonjwa. Antioxidants pia hulinda seli za kinga dhidi ya uharibifu.
3. Inaweza kusaidia kupambana na saratani
Virutubisho kama polyacetylenes, beta carotene na lutein vimeonyesha uwezo wa kupunguza ukuaji wa seli za saratani katika tafiti za maabara na kwa wanyama. Tafiti za awali zinaonyesha manufaa dhidi ya saratani kama leukemia na saratani ya utumbo mpana, ingawa tafiti zaidi kwa binadamu bado zinahitajika.
4. Husaidia kudhibiti sukari kwenye damu
Kiasi kidogo cha juisi ya karoti kinaweza kusaidia kudhibiti sukari kwenye damu. Ina glycemic index ya chini, hivyo haiinui sukari haraka kama vinywaji vingine. Hata hivyo, wagonjwa wa kisukari wanashauriwa kunywa kwa kiasi.
5. Huboresha afya ya ngozi
Vitamini C husaidia uzalishaji wa collagen, ambayo huifanya ngozi iwe imara na yenye mvuto. Beta carotene hulinda ngozi dhidi ya madhara ya mionzi ya jua (UV) na uchafu wa hewa. Pia husaidia kupunguza chunusi na kurekebisha ngozi iliyoharibika.
6. Huimarisha afya ya moyo
Potasiamu iliyopo kwenye juisi ya karoti husaidia kudhibiti shinikizo la damu. Lishe yenye potasiamu nyingi imehusishwa na kupunguza hatari ya shinikizo la damu na kiharusi. Antioxidants pia husaidia kupunguza uharibifu wa mafuta kwenye damu, jambo linalolinda moyo.
7. Hulinda afya ya ini
Carotenoids zilizo kwenye juisi ya karoti zina sifa za kupunguza uchochezi na kulinda ini. Tafiti kwa wanyama zinaonyesha kuwa juisi ya karoti inaweza kupunguza dalili za ini lenye mafuta (fatty liver), ingawa tafiti zaidi kwa binadamu zinahitajika.
#10YrsJembefm #Familiamoja #AhsantekwaTime