Polisi Pwani Wakanusha Taarifa zinazosambaa Mitandaoni

Jeshi la Polisi Mkoa wa Pwani limekanusha vikali taarifa zinazosambaa kwenye mitandao ya kijamii ya Facebook na Instagram zikidai kuwa gari la Polisi lilimgonga na kumuua mwananchi katika eneo la Kongowe, wilayani Kibaha.

Kwa mujibu wa taarifa rasmi iliyotolewa leo Disemba 23 mwaka huu  na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani, ajali hiyo ilitokea Disemba 19 mwaka huu majira ya saa 2:00 usiku katika Barabara ya Morogoro–Dar es Salaam, eneo la Kongowe.

 Ilielezwa kuwa gari ambalo halijatambuliwa namba zake za usajili, likitokea Morogoro kuelekea Dar es Salaam, lilimgonga mwanamke aitwaye Pendo Mugisa Mashauri (20), mkazi wa Kongowe, na kumjeruhi vibaya.

Taarifa hiyo imebainisha kuwa tukio hilo halikuripotiwa mara moja katika kituo chochote cha Polisi, bali liliripotiwa rasmi Disemba 22 mwaka huu majira ya saa 12:00 jioni na shemeji wa marehemu aitwaye Kelvin Leonard.

Baada ya ajali hiyo, wananchi walimkimbiza majeruhi katika Kituo cha Afya cha White Hope kilichopo Miembesaba, Kibaha, ambako alipatiwa huduma ya kwanza kabla ya kuhamishiwa Hospitali ya Rufaa ya Tumbi kwa matibabu zaidi.

Hata hivyo, Jeshi la Polisi limethibitisha kuwa marehemu alifariki dunia Disemba 20 mwaka huu  majira ya saa 9:00 usiku akiwa anaendelea kupatiwa matibabu hospitalini hapo.

Aidha, taarifa hiyo imeeleza kuwa hadi sasa hakuna shuhuda aliyefanikiwa kutambua aina ya gari lililosababisha ajali hiyo, hali iliyopelekea Jeshi la Polisi kuendelea na msako mkali wa kulibaini gari husika.

Jeshi la Polisi Mkoa wa Pwani limewahimiza wananchi kupuuza taarifa zisizo na uthibitisho kutoka kwa mamlaka husika na kuendelea kushirikiana na vyombo vya dola katika kutoa taarifa sahihi zitakazosaidia uchunguzi.

#10YrsJembefm  #Familiamoja #AhsantekwaTime

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii