Wataalamu wa afya wanashauri watu wenye ugonjwa wa mafuta kwenye ini (fatty liver) kuepuka kula baadhi ya vyakula vikiwa vibichi, kwani vinaweza kuathiri ini, kusababisha matatizo ya mmeng’enyo wa chakula au kuongeza hatari ya maambukizi. Baadhi ya vyakula huwa salama na bora zaidi kwa afya ya ini vinapopikwa vizuri.
1. Nyanya
Nyanya mbichi zina kemikali iitwayo solanine, ambayo kwa kiasi kikubwa inaweza kukera mfumo wa mmeng’enyo wa chakula, kwa mujibu wa The Times of India.
Dkt. Akil Palanisamy, daktari wa tiba jumuishi na mwandishi wa kitabu “The T.I.G.E.R. Protocol,” anashauri kuwa kupika nyanya hupunguza kemikali hizi, hivyo kuwa rahisi kumeng’enywa na kuwa salama zaidi kwa afya ya ini.

2. Maembe
Maembe yana kiwango kikubwa cha fructose, aina ya sukari inayochakatwa na ini na kubadilishwa kuwa mafuta. Utafiti wa mwaka 2019 uliochapishwa na Maktaba ya Kitaifa ya Tiba ya Marekani (NLM) unaonesha kuwa ulaji mwingi wa fructose unaweza kusababisha au kuongeza mafuta kwenye ini yasiyotokana na pombe (NAFLD).
Wataalamu wanashauri kula embe moja au mbili ndogo kwa siku, hasa kwa watu wenye matatizo ya ini au kisukari.

3. Matango
Ingawa matango ni salama kwa ujumla, yakiliwa mabichi yanaweza kusababisha kujaa gesi au maumivu ya tumbo kwa baadhi ya watu kutokana na maji mengi na uwezekano wa uchafu wa bakteria.
Kupika matango kidogo au kuyala kwa kiasi kunaweza kusaidia kupunguza usumbufu wa mmeng’enyo wa chakula, jambo muhimu kwa wenye fatty liver.
4. Mayai
Mayai mabichi yana hatari ya kuwa na bakteria wa Salmonella, wanaoweza kusababisha sumu ya chakula.
Kwa watu wenye mafuta kwenye ini, ni muhimu kulinda mfumo wa kinga na kuepuka mzigo wa ziada kwa ini. Kupika mayai vizuri huua bakteria hatari, na kuyafanya kuwa salama na yenye faida kwa afya ya ini.

5. Kuku
Kuku mbichi au aliyeiva nusu anaweza kuwa na bakteria hatari kama Salmonella na Campylobacter wanaoweza kusababisha matatizo ya tumbo na kuathiri afya ya ini.
Kwa mujibu wa Kituo cha Kudhibiti Magonjwa cha Marekani (CDC) Salmonella husababisha visa vingi vya magonjwa yatokanayo na chakula kuliko bakteria wengine, huku kuku akiwa miongoni mwa vyanzo vikuu. Kupika kuku hadi aive vizuri ni hatua muhimu ya kulinda afya.
#10YrsJembefm #Familiamoja #AhsantekwaTime