Ankara — Mkuu wa Majeshi ya Libya Luteni Jenerali Mohammed al-Haddad pamoja na maafisa wengine wanne wa kijeshi wamefariki dunia usiku wa kuamkia leo baada ya ndege waliyokuwa wakisafiria kuanguka muda mfupi baada ya kupaa kutoka mji mkuu wa Uturuki, Ankara.
Waziri wa Mambo ya Ndani wa Uturuki Ali Yerlikaya amethibitisha tukio hilo na kusema kuwa mabaki ya ndege hiyo ya kukodi aina ya Falcon 50 yamepatikana katika wilaya ya Haymana nje kidogo ya mji wa Ankara.
Kwa mujibu wa taarifa za awali, ndege hiyo ilipata hitilafu ya umeme takribani dakika 16 baada ya kuruka, hali iliyomlazimu rubani kuomba kibali cha kutua kwa dharura. Hata hivyo juhudi hizo hazikufanikiwa kabla ya ndege hiyo kuanguka.
Waziri Mkuu wa Libya Abdulhamid Dbeibah, ametoa salamu za rambirambi kufuatia tukio hilo, akieleza masikitiko yake makubwa kwa kifo cha Luteni Jenerali al-Haddad na maafisa wengine waliokuwamo ndani ya ndege hiyo.
Marehemu Mkuu wa Majeshi ya Libya alikuwa nchini Uturuki kwa ziara rasmi ya kikazi, ambapo alikuwa akifanya mazungumzo na viongozi wa juu wa ulinzi wa nchi hiyo. Mapema jana, alikutana na Waziri wa Ulinzi wa Uturuki, Yasar Guler, pamoja na Mkuu wa Majeshi ya Uturuki.
Tukio hilo limeibua mshtuko mkubwa kwa serikali ya Libya na jumuiya ya kimataifa, huku uchunguzi ukiendelea kubaini chanzo kamili cha ajali hiyo.
#10YrsJembefm #Familiamoja #AhsantekwaTime