Yoweri Museveni anaongoza kwa 61.7%

Matokeo ya awali ya uchaguzi wa urais yanaonyesha Yoweri Museveni akiongoza kwa kura 14,232 (61.7%); Bobi Wine anashika nafasi ya pili kwa kura 7,753 (33.64%), kulingana na Tume ya Uchaguzi nchini humo.

Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Simon Mugenyi Byabakama ameyatoa matokeo hayo ya awali kwenye vyombo vya habari, matokeo ambayo yanaelekea kuendeleza utawala wa miongo minne wa Museveni.

Uhesabuji kura unaendelea, upinzani unalaani udanganyifu

Zoezi la uhesabuji kura linaendelea katika maeneo mbalimbali nchini Uganda wakati mtandao wa intaneti umezimwa na kunaripotiwa shutuma za udanganyifu kutoka kwa upinzani kuhusu uchaguzi wa urais na wa wabunge.

"Kesi za kujazwa kwa kura nyingi zinaripotiwa kila mahali," amesema mgombea urais Bobi Wine kwenye mitandao ya kijamii, bila kutoa ushahidi wowote wa maandishi.

Mamlaka hazijajibu madai yake ya udanganyifu wa uchaguzi, wala madai yake kwamba maafisa wengi wa uchaguzi na wasimamizi kutoka chama chake, NUP, "wametekwa nyara, na wengine kufukuzwa kutoka vituo vya kupigia kura."

Kuchelewa kwa hadi saa nne kumehusishwa na hitilafu katika mashine za kibiometriki zinazotumika kuthibitisha utambulisho wa wapiga kura.

Baadhi wamehusisha matatizo haya na kuzimwa kwa mtandao wa intaneti, pamoja na uhaba wa vifaa vya kupigia kura na ucheleweshaji wa uwasilishaji na baadhi ya vituo vya kupigia kura.

Vituo vya kupigia kura vilifungwa baadaye kuliko ilivyopangwa. Tume ya uchaguzi imesema kwamba mtu yeyote aliyejiunga na foleni kabla ya saa 11:00 joni saa za ndani aliweza kupiga kura.

Mapema siku hiyo, tume ya uchaguzi iliomba radhi kwa "matatizo ya kiufundi" na kubainisha kwamba timu zake zilikuwa zikifanya kazi kuyatatua.

Matokeo ya uchaguzi wa rais yatatangazwa Jumamosi saa 10:00 jioni saa za ndani, tume ya uchaguzi imesema

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii