Urusi na China zataka diplomasia ili kuvimaliza vita Ukraine

Urusi na China zimetoa wito wa kuimarishwa kwa juhudi za kidiplomasia ili kufanikisha suluhisho la kudumu kwa vita vya Ukraine.

Hii ni kufuatia mazungumzo kati ya Rais wa Urusi Vladimir Putin na Rais wa China Xi Jinping mjini Beijing.

Katika taarifa ya pamoja iliyotolewa baada ya mkutano huo, mataifa hayo mawili yamesema yanaunga mkono juhudi zote zinazoweza kusaidia kupatikana kwa amani ya kudumu kupitia mazungumzo na diplomasia.

Hata hivyo, China haikuitaka Urusi kusitisha vita ilivyoanzisha dhidi ya Ukraine mwaka 2022, huku Moscow ikiisifu Beijing kwa kile ilichokiita msimamo wa "kati na usioegemea upande.”

Viongozi hao pia wamekubaliana kuongeza ushirikiano wa kijeshi, ikiwemo mazoezi ya pamoja ya anga na majini pamoja na kukabiliana kwa pamoja na vitisho vya kiusalama.

Katika taarifa hiyo, China na Urusi pia zimekosoa mashambulizi ya Marekani na Israel dhidi ya Iran, zikisema hatua hizo zinakiuka sheria za kimataifa na kuhatarisha uthabiti wa Kanda ya Mashariki ya Kati.

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii