Makubaliano ya amani ya Iran yakaribia kukamilika

Rais wa Marekani, Donald Trump, amesema makubaliano ya awali kuhusu amani kati ya Marekani na Iran yako karibu kukamilika, huku matumaini yakiongezeka ya kumalizika kwa vita vilivyodumu kwa miezi mitatu.

Kupitia mtandao wake wa kijamii, Truth Social, Trump amesema makubaliano hayo yanaweza kufungua tena Mlango-Bahari wa Hormuz, njia muhimu ya usafirishaji wa mafuta duniani ambayo imefungwa tangu Marekani na Israel kuanza vita dhidi ya Iran mwezi Februari.

Kwa mujibu wa taarifa mbalimbali, rasimu ya makubaliano hayo inaweka mpango wa hatua kwa hatua wa kusitisha mapigano, kufungua njia ya maji ya Hormuz, na kulegeza vizuizi vya Marekani dhidi ya Iran. Pia kunatarajiwa mazungumzo ndani ya siku 30 hadi 60 kuhusu mustakabali wa hazina ya urani iliyorutubishwa ya Iran, suala ambalo limekuwa kiini cha mvutano.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Marco Rubio, akiwa ziarani India, amesema huenda taarifa zaidi kuhusu makubaliano hayo ikatolewa ndani ya saa chache zijazo.

Hata hivyo Iran imeendelea kusisitiza kuwa haitafuti silaha za nyuklia na inataka kusitishwa kwa mashambulizi mapya, kuondolewa kwa vizuizi vya bandari, na kuondolewa kwa vikwazo vya mafuta. Hata hivyo, maafisa wake wanasema bado kuna masuala yanayohitaji majadiliano kupitia wapatanishi.

10YrsJembefm  #Familiamoja #AhsantekwaTime

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii