Mashirika ya Afya barani Afrika yamesema kuwa mripuko wa ugonjwa wa Ebola katika Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo unaendelea kusambaa kwa kasi katika hatua ambayo haijawahi kushuhudiwa.
Wessam Mankoula anayesimamia kitengo cha dharura na uitikiaji katika kituo cha kudhibiti na kupambana na magonjwa ya miripuko barani Afrika, CDC amesema ugonjwa huo unaambukiza haraka kutokana na kirusi kipya cha Bundibugyo ambacho kimevishinda virusi vyote vinavyosababisha Ebola.
Aidha amesema mripuko wa mwaka 2013 hadi 2016 katika mataifa ya Magharibi mwa Afrika ulikuwa na visa 998 vya Ebola ukilinganisha na hali ya sasa kwamba chini ya miezi mitatu tu tayari visa zaidi ya 1,700 vimeshathibitishwa.
Ingawa ameongeza kuwa kwa sasa wanahitaji dola bilioni 1.4 ili kuendelea kukabiliana na ugonjwa huo hatari. Haya yanajiri wakati Shirika la Afya Ulimwenguni, WHO likisema Ebola hadi sasa imewaangamiza watu 600 data za WHO zinaonesha kuwa visa 1,759 vya ebola vimethibitishwa nchini Kongo tangu mripuko huo ulipotangazwa Mei 15 mwaka huu.